
Taasisi inayojihusisha na utoaji wa elimu kwa watoa huduma katika sekta ya anga, Aerospace Medical and Training Centre (AMTC), inatarajia kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo katika hafla maalum itakayojumuisha maonesho ya maendeleo ya huduma za afya katika sekta ya usafiri wa anga.
Hafla hiyo ambayo inaendana na maadhimisho ya miaka mitano tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo, inatarajiwa kufanyika Aprili 4, 2026 katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam, ikihusisha matukio mbalimbali ikiwemo uzinduzi wa kitabu kinachoitwa “Aviation Guide Book.”
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa AMTC, Dk. Nasra Nassor Omar, kitabu hicho kinatoa mwongozo mfupi na wa vitendo kuhusu huduma ya kwanza katika sekta ya anga, kikilenga wahudumu wa ndege, wafanyakazi wa ardhini, wanafunzi wa mafunzo ya anga pamoja na wadau wengine wa sekta ya usafiri wa anga.
Amesema kitabu hicho kitapatikana kidijitali kupitia majukwaa ya Amazon na Kindle pamoja na majukwaa mengine ya mtandaoni, hatua itakayowezesha wataalamu wa sekta ya anga duniani kote kupata maarifa hayo kwa urahisi.
Akizungumza katika mkutano wake na waandishi wa habari, Dk. Nasra alisema kuwa wakati wa maadhimisho hayo pia kutafanyika uzinduzi wa Mfumo wa Mafunzo na Mitihani Mtandaoni wa AMTC (Online Training Centre) utakaowezesha wataalamu wa sekta ya anga kupata mafunzo ya tiba ya anga, kufanya mitihani na kupata vyeti kupitia simu au kompyuta bila kulazimika kusafiri.
Ameeleza kuwa mfumo huo ni hatua muhimu katika kupanua upatikanaji wa mafunzo ya kitaalamu nchini Tanzania na katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mbali na hilo, AMTC pia imepanga kuendesha kampeni ya uchunguzi wa afya kwa wafanyakazi wa sekta ya anga katika viwanja vikuu vya ndege. Machi 31, 2026 uchunguzi huo utafanyika katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar, ambapo takribani wafanyakazi 200 wa sekta hiyo wanatarajiwa kupata huduma za afya.
Aidha, Aprili 1 hadi 2, 2026 uchunguzi huo utaendelea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam (Terminal 1 na 2), ambapo zaidi ya wafanyakazi 300 wa sekta ya anga watashiriki katika vipimo vya afya pamoja na mafunzo ya uhamasishaji wa afya.
Vipimo vitakavyotolewa ni pamoja na uchunguzi wa shinikizo la damu, sukari kwenye damu, malaria, kiwango cha damu mwilini pamoja na uhamasishaji na uchunguzi wa awali wa saratani ya shingo ya kizazi, saratani ya matiti na saratani ya tezi dume.
Dk. Nasra amesema hatua hizo zinalenga kusaidia kugundua changamoto za kiafya mapema na kulinda afya ya wafanyakazi wa sekta ya anga, akisisitiza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha wataalamu wa sekta hiyo wanakuwa na mafunzo sahihi, afya bora na uwezo wa kukabiliana na dharura ili kulinda usalama wa abiria na wafanyakazi wote wa sekta hiyo.
“Tunawaalika wadau wote wa sekta ya anga, mashirika ya ndege, waendeshaji wa viwanja vya ndege, mamlaka za udhibiti, washirika wa sekta ya afya pamoja na vyombo vya habari kushiriki nasi katika hatua hii muhimu. Kwa pamoja tunaweza kuendelea kuimarisha afya na usalama wa sekta ya usafiri wa anga nchini Tanzania na katika ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Dk. Nasra.
AMTC ambayo mwaka huu inaadhimisha miaka mitano tangu kuanzishwa kwake, imejikita katika uchunguzi wa afya kwa wataalamu wa anga kabla ya kupata leseni za kuruka, utoaji wa mafunzo ya tiba ya anga, maandalizi ya huduma za dharura (First Aid) pamoja na kuimarisha afya na ustawi wa wafanyakazi wa sekta ya usafiri wa anga nchini.
“Fikiria hali ambapo abiria anapata mshtuko wa moyo ndani ya ndege ikiwa futi 35,000 juu angani. Katika wakati huo maisha yake yanaweza kutegemea uwepo wa mhudumu wa ndege au mtaalamu aliyepata mafunzo sahihi ya huduma ya kwanza na ufufuaji wa mapigo ya moyo na mapafu (CPR). Maarifa haya yanaweza kuleta tofauti kati ya uhai na kifo,” alisisitiza.
Alisema hiyo ndiyo sababu kuu iliyoisukuma taasisi hiyo kuanzishwa, ili kuhakikisha wataalamu wa sekta ya anga wanakuwa na maandalizi sahihi ya kitabibu na uelewa wa kukabiliana na dharura kwa ajili ya kulinda usalama wa abiria, wafanyakazi na jamii kwa ujumla.







Social Plugin