Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

‎KIJAJI ATAKA NGORONGORO ILINDWE ZAIDI, HUDUMA ZA UTALII ZABORESHWA

  

Na Bora Mustafa - Arusha

‎Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji,  ametoa maagizo kwa Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Kamishna Abdul Razaq Badru, kuhakikisha hifadhi ya Ngorongoro inalindwa kikamilifu ili iendelee kuwa na ikolojia yenye mvuto na kuhifadhi rasilimali zake zote za asili.

‎Dkt. Kijaji ametoa maagizo hayo Januari 29, 2026 wakati wa hafla ya kuvishwa cheo cha Ukamishna wa Uhifadhi pamoja na uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa NCAA, iliyofanyika jijini Arusha.

‎Amesema pamoja na ulinzi wa hifadhi, huduma za malazi zinaendelea kuboreshwa ili kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya utalii, hatua itakayoongeza idadi ya vitanda kutoka 1,500 vya sasa hadi zaidi ya 2,000.


‎Aidha, amemtaka Kamishna kushirikisha wadau mbalimbali katika kubuni na kuibua mazao mapya ya utalii pamoja na kuyatangaza, hususan kwa taasisi za utalii zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, akisisitiza kuwa angalau kila mwaka kuwe na kivutio kimoja kipya cha utalii kinachoingizwa sokoni.


‎Waziri huyo pia amesisitiza umuhimu wa kuboresha huduma za utalii kwa ujumla ili kuongeza idadi ya wageni na kufikia matarajio yaliyojiwekea sekta hiyo, sambamba na kuimarisha mahusiano kati ya jamii zinazozunguka hifadhi na mamlaka, ili wananchi wanufaike na rasilimali zinazopatikana katika Hifadhi ya Ngorongoro.

‎Amesema Mheshimiwa Rais ameridhishwa kwa kiwango kikubwa na ushirikiano uliotolewa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika mwaka 2025, na kupitia yeye amemtuma awafikishie salamu za pongezi, akisisitiza kuwa ushirikiano huo pamoja na umoja uendelee kudumishwa ndani ya Mkoa wa Arusha.

‎DC Mkude pia amempongeza Kamishna Abdul Razaq Badru kwa kuvikwa cheo siku ya leo, akibainisha kuwa Mkoa wa Arusha upo salama na utaendelea kushirikiana kwa karibu na NCAA katika utekelezaji wa majukumu ya maendeleo, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuyaishi na kuyatekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika falsafa ya 4R.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com