Na Bora Mustafa, Arusha.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, ameongoza hafla ya kuvishwa cheo Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa Bw. Abdul Razaq Badru, pamoja na uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi wa mamlaka hiyo.
Hafla hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha mifumo ya uongozi na usimamizi wa uhifadhi, sambamba na kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa taifa.
Akizungumza katika hafla hiyo Januari 29, 2026 , Dkt. Kijaji amezielekeza taasisi zote za utalii nchini kuandaa mipango mahsusi ya kutumia matukio makubwa ya kitaifa na kimataifa kama fursa ya kuongeza mapato, kuvutia watalii wengi zaidi na kunufaika kiuchumi, huku akisisitiza umuhimu wa ubunifu na maandalizi ya mapema katika sekta hiyo.
Aidha, Waziri huyo amezitaka taasisi za uhifadhi kuongeza idadi ya vitanda vya malazi katika maeneo ya uhifadhi kutoka vitanda 1,500 vilivyopo sasa hadi kufikia zaidi ya vitanda 2,000, hatua inayolenga kukidhi ongezeko la watalii, kuongeza muda wa watalii kukaa nchini na kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa.
Dkt. Kijaji pia amesisitiza umuhimu wa uhifadhi endelevu unaozingatia maslahi ya jamii zinazozunguka hifadhi, akibainisha kuwa maendeleo ya utalii yanapaswa kwenda sambamba na uhifadhi wa mazingira pamoja na ustawi wa wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NCAA, Jenerali Mstaafu Venancy Mabeo, amezisisitiza taasisi za utalii kuwa tayari wakati wote, akieleza kuwa mafanikio ya sekta ya utalii hayategemei vivutio pekee bali pia usalama, amani na utulivu wa nchi, ambavyo ni msingi wa kuendelea kuvutia watalii kutoka ndani na nje ya nchi.
Pia Kwa upande wa wadau wameeleza matumaini yao kuwa uongozi mpya utaongeza ufanisi katika uhifadhi wa rasilimali za asili na kukuza sekta ya utalii kwa tija zaidi.




















Social Plugin