Na Bora Mustafa,
Arusha
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Mhe. Joseph Mkude, amewahimiza wananchi kuzingatia afya zao kwa kufanya uchunguzi wa mara kwa mara ili kugundua magonjwa mapema, akibainisha kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kupunguza vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza.
Mhe. Mkude ametoa wito huo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kambi Maalum ya Uchunguzi na Matibabu ya Magonjwa ya Moyo inayofanyika katika Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC), ambapo amesema kuwa magonjwa ya moyo, shinikizo la damu na kisukari yameendelea kuathiri wananchi wengi, huku takwimu zikionyesha kuwa asilimia 32 ya vifo vinatokana na magonjwa ya moyo.
Katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kupata huduma za uchunguzi na matibabu zinazotolewa katika kambi hiyo, akieleza kuwa uchunguzi wa mapema huongeza nafasi ya kupona na kuokoa maisha.
Akizungumzia suala la Bima ya Afya, Mhe. Mkude amesema kuwa kujiunga na bima ni suluhisho muhimu la changamoto ya gharama za matibabu kwa wananchi wengi.
Amesema wananchi wengi wamekuwa wakipata mshtuko wa kifedha wanapougua kutokana na kutokuwa na bima, hali inayoweza kuepukika kwa kujiunga na mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unaosimamiwa na Serikali.
Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa bima ya afya katika Jiji la Arusha, ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma za afya bila kikwazo cha gharama, hasa kwa magonjwa yanayohitaji matibabu ya muda mrefu.
Aidha, Mhe. Mkude amebainisha kuwa juhudi za Serikali katika kuimarisha michezo na afya zitaendelea, akitaja maandalizi ya mashindano ya AFCON yanayotarajiwa kufanyika jijini Arusha mwakani kama sehemu ya kuhamasisha jamii kuishi maisha yenye afya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisegi, amemshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kutembelea kambi hiyo na kuunga mkono juhudi za kuboresha huduma za matibabu ya moyo.







Social Plugin