Na Mwandishi Wetu Malunde 1 Blog
Katika kuimarisha utoaji wa haki na huduma kwa wananchi, Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Dkt. Juma Zuberi Homera, amezindua rasmi huduma ya utoaji wa vyeti vya kuzaliwa ndani ya masaa 48.
Akizungumza wakati wa ziara yake katika Taasisi ya Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Dkt. Homera amesema mpango huo utarahisisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi na kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa wakati, hatua ambayo itachangia kuimarisha uchumi wa taifa.
Dkt. Homera amesema masuala kama ndoa, vifo na mirathi yote yanahitaji vyeti ili wananchi waweze kupata stahiki zao, hivyo mpango huo wa masaa 48 utapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto zilizokuwa zikijitokeza.
Amebainisha kuwa utekelezaji wa mpango huu ni sehemu ya maelekezo ya Mheshimiwa Rais, unaolenga kuhakikisha haki inapatikana kwa haraka na ufanisi kwa Watanzania wote.
Katika ziara hiyo, Waziri Homera pia ametembelea Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali pamoja na Roscoe of Tanzania, ambako amezindua magari mapya matatu yaliyotolewa na serikali—mawili kwa ajili ya wakuu wa taasisi na moja kwa matumizi ya wananchi pamoja na watumishi.
Aidha, amewataka viongozi kuhakikisha wanatoa matamko yenye msingi wa utafiti ili kuepusha hasara na migogoro ya kisheria inayoweza kujitokeza kutokana na kauli zisizo sahihi.
Akiwa katika Shule ya Sheria Tanzania, Dkt. Homera amewasisitiza watendaji kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu, kuacha masilahi binafsi na kuhakikisha taaluma ya sheria inasimamiwa kwa weledi.
Pia amehimiza matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma, akisisitiza kuwa mifumo ya kielektroniki itasaidia kuharakisha upatikanaji wa haki na kuongeza ufanisi katika taasisi za kisheria nchini.





Social Plugin