Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetoa taarifa yake kwa Vyombo vya habari kuhusu hali ya usalama nchini kwa kipindi cha saa sita tangu ilipotoka taarifa ya awali majira ya saa 6 mchana leo Jumanne Disemba 09, 2025.
Kulingana na Msemaji wa Polisi, Makao Makuu Dodoma, David Misime amesema hali ya usalama nchini imeendelea kuwa shwari na Vyombo vya Ulinzi na Usalama vimeendelea kuimarisha usalama nchini, pamoja na kulinda raia na mali zao hadi muda huu wa jioni.
"Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya ulinzi na usalama vingependa kuwahakikishia kuwa kuanzia majira haya vitaimarisha zaidi ulinzi na usalama tunapoelekea usiku ili kuzuia na kudhibiti vitendo vyovyote vinavyoweza kuwa ni tishio la kiusalama." Amesema Kamanda Misime.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa kila mwananchi kuendelea kuzingatia kanuni za kiusalama na kuendelea kutii sheria za nchi kwani kila mmoja anahitaji kuwa salama wakati wote.

Social Plugin