Ofisi ya Kata Mkongo Gulioni ambayo ambayo Waziri wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo daktari Juma Zuberi Homera ametimiza ahadi yake ya kutoa bati 100 zenye thamani ya Sh.milioni mbili na laki tano kwaajili ya kuezeka ofisi hiyo Na Regina Ndumbaro-Namtumbo
Waziri wa Katiba na Sheria ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Dkt. Juma Zuberi Homera, ametekeleza ahadi yake ya kuchangia bati 100 zenye thamani ya shilingi 2,500,000 kwa ajili ya kupaua jengo la Ofisi ya Kata ya Mkongo Gulioni.
Ahadi hiyo aliitoa tarehe 14 Oktoba 2025, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuharakisha maendeleo ya miundombinu ya utawala katika kata hiyo.
Makabidhiano ya bati hizo yamefanyika kupitia kwa mwakilishi wake, Mwalimu Saidi Homera, ambaye ameeleza kuwa wananchi wa Mkongo Gulioni walikuwa tayari wametumia nguvu kazi kufanikisha ujenzi katika hatua ya kenchi.
Hata hivyo, kutokana na kuanza kwa mvua, kulitarajiwa hatua ya haraka ya kupaua jengo hilo ili liweze kukamilika na kuanza kutoa huduma bila vikwazo.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mkongo Gulioni, Ndugu Joseph Ngongi,kwa niaba ya wananchi wake ameushukuru uongozi wa Mbunge huyo kwa kutimiza ahadi kwa wakati.
Amesema kuwa kukamilika kwa jengo hilo kutawasaidia watumishi wa serikali kupata ofisi bora, tofauti na ofisi ya sasa ambayo ni chakavu na haikidhi mahitaji ya utoaji huduma.
Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Namtumbo imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na wananchi katika miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu ya kijamii na kuongeza ustawi wa wananchi wa Namtumbo kwa ujumla.

Social Plugin