Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAMCU LTD YAZINDUA MRADI WA MAGARI YA SHILINGI 1,150,000,000 KWA AJILI YA BIASHARA NA MAENDELEO YA WANANCHI TUNDURU

Magari ya chama kikuu cha Ushirika TAMCU LTD yakiwa yamewasili katika ofisi za chama hicho Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kabla ya mgeni rasmi  mkuu wa Wilaya ya Tunduru Denis Masanja kukata utepe kuyazindua rasmi

Na Regina Ndumbaro Tunduru 

Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU LTD) kimezindua rasmi mradi wa magari matano yenye thamani ya shilingi  1,150,000,000 katika hafla iliyoanza kufanyika katika kijiji cha Nakapanya, Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru mpaka Ofisi kuu ya TAMCU LTD 

Hafla hiyo imehudhuriwa  na mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Denis Masanja,na viongozi mbalimbali wa serikali na chama chini ya uratibu wa Mtendaji Mkuu wa TAMCU LTD, Marcelino Mrope, huku wananchi, wanachama na wadau mbalimbali wakihudhuria.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya  ya Tunduru Denis Masanja amesema magari hayo yatumike kwa madhumuni ya kibiashara ili kuongeza kipato cha chama na wananchi kwa ujumla. 

Amesisitiza kuwa mradi huo utafungua fursa za ajira kwa vijana wa Wilaya ya Tunduru na kusaidia kuchochea uchumi wa eneo hilo. 

Aidha, amewataka madereva watakaoajiriwa kufuata sheria za barabarani, akionya kuwa itakuwa aibu kwa lori la TAMCU kuhusishwa na vitendo vya uhalifu kama usafirishaji wa bangi, wahamiaji haramu au magendo.

Masanja ameongeza kuwa uwepo wa magari hayo utawasaidia wadau mbalimbali kusafirisha pembejeo za kilimo kama mbolea na viuatilifu kwa urahisi zaidi, jambo litakalosaidia kuongeza uzalishaji. 

Pia ametoa wito kwa vyama vya msingi (AMCOS) kuhakikisha kila chama kinamiliki chombo cha usafiri ili kujiimarisha kiuchumi. 

 Amesema magari matano yanaweza kuonekana kama hatua ndogo, lakini kwa TAMCU ni hatua kubwa ya maendeleo, na amewatakia wananchi wote heri ya Sikukuu ya Krismasi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAMCU LTD, Musa Manjaule, amesema uzinduzi huo ni wa magari mawili yaliyowasili awali, huku magari mengine matatu yakitarajiwa kufuata baadaye. 

Ameeleza kuwa wanachama walikubaliana kununua magari matano, na kwa bahati nzuri yote tayari yamenunuliwa. 

Amekumbusha historia ya chama hicho, akisema zamani kilijulikana kama RSU Songea kabla ya kugawanywa mwaka 1994 na kuanzishwa TAMCU ikiwa na AMCOS 10 pekee.

Manjaule amekiri kuwa TAMCU iliwahi kukumbwa na changamoto nyingi zilizokifanya chama hicho kuyumba, lakini akasema kila jambo lina wakati wake.

Ameeleza kuwa bodi za awali zilirekebisha misingi, na bodi ya sasa imejipanga kusimama imara na kuleta matokeo chanya kwa wanachama na jamii.

 Ametoa wito wa kutokukata tamaa, akisisitiza kuwa changamoto ni sehemu ya safari ya maendeleo, na ameahidi kuwa wanachama na wananchi wataona mambo makubwa zaidi yakifanyika kupitia TAMCU kwa kuzingatia misingi saba ya Ushirika na wajibu wa kusaidia jamii.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com