Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Msimu wa Krismasi umekuwa wa neema kwa wazee na wasiojiweza katika Kituo cha Kolandoto, Manispaa ya Shinyanga, baada ya mdau wa maendeleo, Mhandisi James Jumbe, kuamua kusherehekea nao kwa kuwapa zawadi na mahitaji mbalimbali, ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wao na kuwapa faraja katika umri wao wa uzee.
Mhandisi Jumbe ametoa msaada wa mahitaji mbalimbali ikiwa ni sehemu ya kusherehekea Sikukuu ya Krismasi leo tarehe 25 Desemba,2025.
Zawadi hizo muhimu kwa ajili ya Sikukuu zinalenga kuwaenzi wazee na kuhakikisha hawajihisi wapweke, bali wanajiona kuwa ni sehemu muhimu ya jamii inayopendwa na kuthaminiwa.
Zawadi hizo zimekabidhiwa kwa niaba yake na Ndg. Derick Peter, ambaye amesisitiza kuwa kuwajali wazee si hiari, bali ni wajibu wa kijamii.
Akizungumza katika kituo hicho, Ndg. Derick Peter, kwa niaba ya Mhandisi Jumbe, ameeleza kuwa msimu huu wa Krismasi umekuwa fursa ya kipekee kwa Mhandisi kugusa maisha ya wazee hawa kwa vitendo.
"Katika kusherehekea Sikukuu hii ya Krismasi, Kijana wenu Mhandisi James Jumbe ameona ni vyema kurudi kwa wazee wetu na makundi maalum ili kuwapa faraja. Tumefika hapa kusherehekea nao kwa pamoja, kwani heshima na matunzo kwa wazee ni baraka kwa jamii nzima. Ni muhimu kuwafariji na kuwapatia mahitaji haya ili msimu huu uwe wa furaha kwao pia," amesema Derick.
Derick amebainisha kuwa utaratibu wa Mhandisi Jumbe kukumbuka wazee na wasiojiweza ni kielelezo cha moyo wake wa kutoa na upendo wa dhati kwa watu wa Shinyanga.
"Hii siyo mara ya kwanza kwa Mhandisi kufanya hivi; mwaka uliopita tulileta mahitaji, na safari hii pia siyo mwisho. Tutaendelea kuwa karibu nao, kutoa misaada, na kuwatia moyo wazee wetu ili wajue kuwa tunawathamini na kuthamini mchango wao katika maisha yetu," ameongeza Derick.











Social Plugin