Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JENISTA MHAGAMA AAGWA PERAMIHO TAIFA LITAKUMBUKA MCHANGO WAKE WA UMOJA NA UADILIFU

Jeneza la aliyewahi kuwa Waziri wa Afya na Mbunge wa Jimbo la Peramiho Jenista Mhagama likiwa limebebwa kwaajili ya kufanyiwa ibada katika kanisa la Abasia Peramiho 

Na Regina Ndumbaro-Peramiho 

Aliyewahi kuwa Waziri wa Afya na Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Jenista Mhagama, amefanyiwa ibada ya kuagwa leo Desemba 15 katika Kanisa Katoliki Abasia Peramiho mkoani Ruvuma. 

Marehemu alifariki dunia mkoani Dodoma alipokuwa akitekeleza majukumu yake ya kibunge baada ya kuapishwa, na baadaye mwili wake kusafirishwa hadi Ruvuma. 

Mwili wa marehemu utalala leo nyumbani kwake Parangu Peramiho, huku mazishi yakipangwa kufanyika kesho katika kijiji cha Luanda wilayani Mbinga, alikozikwa marehemu mume wake.

Ibada hiyo ya kuagwa imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na chama, akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, Spika wa Bunge Mheshimiwa Mussa Hassan Zungu, pamoja na aliyewahi kuwa Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson, pamoja na viongozi wengine wa kitaifa na kidini. 

Viongozi hao walikusanyika Peramiho kutoa heshima za mwisho kwa marehemu ambaye amekuwa na mchango mkubwa katika uongozi wa taifa.

Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema marehemu Jenista Mhagama alikuwa kiungo muhimu kati ya serikali na taasisi za kidini.

 Amesema Rais amemtuma kuwahakikishia wananchi kuwa serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini ili kuendeleza heshima ya Tanzania katika misingi ya umoja wa kitaifa, uhuru wa kuabudu, amani na usalama. 

Ameongeza kuwa marehemu alikuwa mpatanishi mahiri kati ya serikali na wafanyakazi, sekta binafsi na serikali, na alifanya kazi hiyo kwa uadilifu mkubwa huku akitanguliza imani ya dini katika maisha yake.

Kwa upande wa wananchi wa Peramiho akiwemo Lucas Ngonyani na Salome Nyalende wamesema wameshtushwa na kusikitishwa na msiba huo mzito, wakieleza kuwa marehemu Jenista Mhagama alikuwa mtu wa watu, mnyenyekevu, msikivu na aliyejitoa kwa rika zote. 

Wamesema alitekeleza kwa vitendo ahadi zake kwa wananchi hususani katika mikopo kwa vijana, miundombinu ya barabara, umeme na maji, na hivyo pengo lake ni kubwa sana. 

Wananchi hao wameomba atakayechukua nafasi yake aige mfano wa uongozi na utumishi aliouonesha marehemu enzi za uhai wake.





Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com