Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Katika jitihada za kulinda thamani ya Shilingi na kupunguza gharama ambazo Serikali hutumia katika kuchapisha fedha mpya, wananchi wameshauriwa kuwa na uelewa mpana juu ya alama za usalama zinazopatikana kwenye noti halisi pamoja na mbinu za kuzitunza kwa usahihi.
Hayo yamebainishwa leo
Novemba 21, 2025 jijini Dodoma na Afisa Mwandamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Atufigwege Jampion Mwakabalula katika mafunzo maalum kwa waandishi wa habari kuhusu namna ya kutambua alama za usalama kwenye noti ambapo ameeleza kuwa bado kumekuwepo na changamoto ya baadhi ya watu kutumia fedha zisizo halali kutokana na kukosa uelewa wa alama za kiusalama zinazowekwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Amezitaja Alama Muhimu za Kutambua Noti Halisi kuwa kila noti ya Tanzania ina alama za kiusalama ambazo ni vigumu kuiga, zikiwemo kivuli cha picha (Watermark) kinachoonekana ukitazama noti dhidi ya mwanga na namba ya usalama (Security Thread) inayong'aa au kubadilika rangi wakati wa kugeuza noti.
Alama nyingine ni rangi zinazong’aa (Optically Variable Ink) zinazobadilika kulingana na mwanga,Vibambo vya kuhisika kwa vidole (Raised Print) vinavyoweza kuhisiwa kwa kugusa sehemu fulani za noti na kufafanua kuwa utambuzi wa alama hizo husaidia wananchi kuepuka kudanganywa na noti bandia ambazo mara nyingi huwa na makosa madogo madogo yanayoonekana ukichunguza kwa makini.
Amesema Matumizi ya Noti Bandia Yanaigharimu Serikali kwa kuwa matumizi ya noti hizo huathiri uchumi kwa kuharibu mzunguko sahihi wa fedha, na pili, Serikalini hulazimika kutumia fedha nyingi kuchapisha noti mpya ili kuchukua nafasi ya noti ambazo hazifai kutumika.
Kwa mujibu wa Mwakabalula, gharama hizo zingeweza kuelekezwa kwenye sekta za jamii kama afya, elimu na miundombinu endapo kila mwananchi angezingatia utunzaji sahihi wa fedha na kutoa taarifa mapema pindi wanapohisi uwepo wa noti bandia kwenye mzunguko.
Kuhusu namna Bora ya Kutunza Fedha
amesema wananchi wanatakiwa kutozikunja noti mara kwa mara,Kuzitunza kwenye pochi au kwenye pochi ya simu isiyobana,Kutoweka noti sehemu zenye maji, joto kali au unyevunyevu na Kuepuka kuchora, kutoboa au kuweka alama kwenye noti.




Social Plugin