Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHIRIKA LA YAWE LAWAKUTANISHA VIJANA WA SHINYANGA KUJADILI NAMNA YA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI



Na Abel Michael

Mkoa wa Shinyanga umeendelea kuwa miongoni mwa maeneo nchini yanayokumbwa na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi, hatua inayotokana na uharibifu wa misitu uliofanywa na vizazi vilivyopita kwa ajili ya shughuli za kibinadamu kama vile ufugaji, kilimo na matumizi ya kuni. Uharibifu huo umechangia kupungua kwa mvua za uhakika na kusababisha ongezeko la ukame.

Katika jitihada za kukabiliana na hali hiyo, Shirika lisilo la Youth And Woman Emancipation (YAWE) limewakutanisha kundi la vijana wa manispaa ya Shinyanga kujadili mikakati ya kuimarisha uhifadhi wa mazingira, ikiwemo kupanda miti na kutoa elimu juu ya utunzaji wa mazingira ndani ya jamii.

Afisa Mazingira wa Manispaa ya Shinyanga, Ezra Manjelenga, amesema mabadiliko ya tabianchi yamekuwa na athari za kijamii ikiwemo mauaji ya vikongwe yaliyoshuhudiwa miaka ya 2000, ambayo yalihusishwa na imani potofu wakati chanzo kikuu kikiwa ni uharibu wa mazingira na matumizi ya nishati zisizo safi kama kuni katika kupikia majumbani.

Kwa upande wake, Afisa Utamaduni wa Manispaa ya Shinyanga, Charles Luchagula, amewataka vijana kuchangamkia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kupitia mapato ya ndani ya halmashauri kwa kuanzisha vikundi na kutekeleza miradi ya kimazingira itakayowawezesha kulinda mazingira na kukuza uchumi wao.

Aidha, Afisa Maendeleo ya Jamii, Salome Komba, amesema mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuwa daraja la ukuaji wa kiuchumi kwa vijana endapo watatumia fursa zilizopo kuanzisha miradi endelevu inayohusiana na uhifadhi wa mazingira.

Hata hivyo, baadhi ya vijana walioshiriki kikao hicho wameeleza changamoto zinazowazuia kushiriki kikamilifu katika masuala ya mazingira, ikiwemo ukosefu wa majukwaa mahsusi yanayowaunganisha vijana kujadili masuala ya mazingira na ushiriki mdogo kwenye kamati za mazingira za vijiji na mitaa.

Awali, Msimamizi wa Shirika lisilo la Kiserikali YAWE, Moshi Jilalage, alisema kikao hicho kililenga kutoa nafasi kwa vijana kujadili ajenda za mazingira na kufikia maazimio ya pamoja. Miongoni mwa maazimio hayo ni pamoja na kuanzishwa kwa klabu za vijana zitakazoshughulikia shughuli za uhifadhi wa mazingira na kufufua kamati za mazingira katika ngazi za jamii.














Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com