Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesisitiza umuhimu wa kuimarisha ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha nchini, ikibainisha kuwa ulinzi huo ni msingi muhimu wa uthabiti wa mifumo ya kifedha na usawa katika soko.
Afisa Sheria Mwandamizi wa BoT, Ramadhan Myonga, amesema ulinzi wa mteja ni muunganiko wa sheria, sera, taratibu na taasisi zinazolenga kuhakikisha haki za watumiaji zinalindwa na kwamba watoa huduma wanatoa bidhaa kwa uwazi, usahihi na bila mbinu za udanganyifu.
Akizungumza na Waandishi wa habari Novemba 202,2025 Jijini Dodoma Myonga ameeleza kuwa Kanuni za BoT za mwaka 2019 kuhusu Kumlinda Mtumiaji wa Huduma za Kifedha ndizo zinazoongoza ulinzi huo, kwa kuhakikisha watumiaji wanapata taarifa sahihi kabla ya kufanya maamuzi ya kifedha.
Amesema maboresho haya yametokana na mafunzo yaliyotokana na mgogoro wa kifedha wa mwaka 2007 hadi 2008 ambapo ilionekana wazi kwamba upungufu wa ulinzi wa wateja nchini Marekani ulikuwa miongoni mwa vichocheo vya kuvurugika kwa mifumo ya kifedha duniani.
Katika muktadha wa kimataifa, Myonga amesema nchi nyingi zimechukua hatua za kisera na kisheria kuimarisha usimamizi wa soko huku akitolea mfano wa nchi ya Marekani kuwa ilipitisha Sheria ya Dodd-Frank ya mwaka 2010 na kuanzisha taasisi maalum ya CFPB yenye dhamana ya kumlinda mtumiaji wa huduma za kifedha, huku Uingereza ikiunda mamlaka ya FCA mwaka 2012 kusimamia mwenendo wa soko na masuala ya haki za watumiaji.
Vilevile, amebainisha kuwa mataifa mengi yanayoendelea, ikiwemo Zambia, yamefanya marekebisho ya sheria ili kuongeza masharti ya ulinzi kwa wateja wa huduma za kifedha.
Myonga ameongeza kuwa miongozo ya Umoja wa Mataifa kuhusu ulinzi wa watumiaji imeboreshwa pia kujumuisha maeneo muhimu yanayotikisa sekta ya kifedha ikiwemo uwazi, mwenendo wa biashara, ulinzi wa taarifa binafsi za wateja, elimu ya kifedha na utatuzi wa malalamiko.
Amesema miongozo hiyo imekuwa rejea muhimu kwa nchi zinazoimarisha mifumo ya uwajibikaji katika sekta ya fedha.
Amesisitiza kuwa Tanzania inaendelea kuchukua hatua za kulinda watumiaji kwa kuimarisha usimamizi wa taarifa, udhibiti wa mwenendo wa watoa huduma, kujenga uelewa wa kifedha kwa wananchi na kuhakikisha wateja wanapata huduma bila unyanyasaji, udanganyifu au matumizi ya mbinu zisizo za haki.
Myonga amesema hatua hizi zimekusudiwa kuongeza imani ya umma katika sekta ya fedha, kukuza ujumuishaji wa kifedha na kuhakikisha wananchi wanatumia huduma kwa usalama na uelewa sahihi.




Social Plugin