
Na Mwandishi Wetu.
Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Shinyanga kinafanya mahafali ya kwanza kwa wahitimu wa programu maalum ya Wanawake na Samia, ambapo jumla ya wanawake 81 wanahitimu mafunzo ya ufundi bure katika fani mbalimbali.
Mahafali hayo yamefanyika
leo Oktoba 2, 2025, yakihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita,
ambaye amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha programu hiyo
inayowawezesha wanawake kupata ujuzi wa ufundi na kujikwamua kiuchumi.
“Mafunzo haya
yanawajengea uwezo wa kujiajiri na kuimarisha uchumi wa familia zenu, hivyo
natoa rai kwa wahitimu kuunda vikundi vya ujasiriamali ili wanufaike na mikopo
isiyo na riba inayotolewa na Halmashauri kwa asilimia 10, ambapo wanawake
wananufaika kwa asilimia nne. Pia anawasihi kutumia fursa za mikopo na miradi
inayotolewa na taasisi mbalimbali za kifedha”, amesema Mhita.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Samia Taifa, Futuma Madidi, amemshukuru
Rais Samia kwa kuanzisha programu hiyo, huku akiomba serikali iwape wahitimu
vipaumbele katika zabuni na fursa nyingine za kiuchumi.
Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga,
Abraham Mbughuni, amebainisha kuwa wahitimu hao wamesoma fani mbalimbali
ikiwamo ushonaji (26), saluni (25), umeme (10), bomba (7), udereva (4), mapambo
(4), mapishi (3) na kompyuta (2).
Baadhi ya wahitimu akiwamo Zainabu Joseph wanamshukuru Rais Samia kwa kuwapatia nafasi ya kujifunza bure, wakisema ujuzi huo unawasaidia kuendesha maisha na kujipatia kipato.
<<<TAZAMA PICHA MATUKIO MBALIMBALI>>>
Social Plugin