
Katika kuelekea maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja, wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) mkoa wa Shinyanga wamefanya tukio la kipekee la kutoa huduma kwa jamii, kwa kutembelea Gereza la Wilaya ya Shinyanga na kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali kwa wafungwa walioko gerezani.
Katika tukio hilo la kugusa maisha ya
wenzetu wanaopitia changamoto, NSSF imetoa msaada wa vitu muhimu zikiwemo sabuni, miswaki, mafuta, nguo, pamoja na
vifaa vya kufanyia usafi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada
huo, Meneja wa NSSF Mkoa wa Shinyanga,
Bi. Amina Mdabi, alisema kuwa lengo la tukio hilo ni kurudisha kwa jamii
na kutambua kuwa hata wale walioko magerezani bado ni sehemu ya jamii, na
wanapaswa kuonjeshwa upendo na mshikamano wa kijamii.
“Tunajua kuwa wenzetu walioko ndani
bado ni sehemu ya jamii yetu. Mwisho wa siku, watarejea uraiani na kuendelea na
maisha yao kama kawaida. Tumezungumza nao na kuwaeleza kuwa hata wao wana
nafasi ya kujiunga na NSSF, ili waanze kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha yao
ya sasa na baadaye,” alisema Mdabi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Shinyanga, Bw.
Kizito Kunambi, alitoa shukrani kwa NSSF kwa msaada huo, akibainisha
kuwa si kila mfungwa anayeingia gerezani ana familia au ndugu wa kumsaidia.
“Tunashukuru sana kwa msaada huu.
Serikali peke yake haiwezi kugharamia kila kitu, na ukweli ni kwamba baadhi ya
waliopo hapa hawana ndugu kabisa. Msaada huu utasaidia kuleta utulivu, faraja
na kuimarisha hali ya kisaikolojia ya wafungwa wetu,” alisema Kunambi.
Tukio hili ni sehemu ya mikakati ya NSSF ya kuimarisha uhusiano na jamii, sambamba na kuhamasisha umuhimu wa hifadhi ya jamii kwa kila Mtanzania – bila kujali hali yake ya sasa. Katika Wiki ya Huduma kwa Mteja, NSSF inaendelea kuonyesha kuwa huduma kwa wateja si tu ofisini, bali ni pia kujali ustawi wa jamii nzima.




























Social Plugin