Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ameshirikiana na wananchi wa Kijiji cha Msanga katika ujenzi wa Kituo cha Afya Msanga wilayani Chamwino huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi na wananchi katika kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati, Wananchi wapate huduma bora za afya na kwa wakati.
Hayo yamejiri leo Sept 15 ,2025 alipotembelea Kijiji cha Msanga kikichopo tarafa ya Chilonwa Wilayani Chamwino ambapo amepongeza juhudi za ujenzi wa Kituo hicho na kusisitiza kuwa mradi huo lazima ukamilike kwa wakati ili wananchi wapate huduma bora za afya karibu na makazi yao.
Amesema lengo la Serikali ni kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua pamoja na kupunguza gharama zinazotokana na wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Chamwino.
Senyamule amemtaka mkandarasi kuongeza kasi na kukamilisha mradi mwezi Desemba mwaka huu na ikibidi kabla ya muda uliopangwa ili kuwapunguzia adha wanachii hao.
Aidha kituo kiasi cha shilingi milioni 250 zilitolewa na Serikali Kuu mwezi Juni mwaka huu, zikilenga kujenga jengo la mama na mtoto, vyoo vya wagonjwa, eneo la kuchomea taka na kuweka msingi wa jengo la upasuaji ambapo Kwa sasa, jengo la mama na mtoto lipo katika hatua ya msingi kwa asilimia tano, huku maandalizi ya majengo mengine yakiendelea.
Kituo cha Afya Msanga kinatarajiwa kuhudumia zaidi ya wananchi 7,000, wakiwemo wanawake 3,952 na wanaume 3,698, pamoja na vijiji jirani.
Kwa upande wa hali ya upatikanaji wa dawa imeelezwa kufikia asilimia 95, ingawa kituo kinahitaji watumishi watatu zaidi ili kukidhi mahitaji.
Kutokana na hayo Wananchi wa Kijiji cha Msanga wameeleza matumaini yao kwa ujenzi huo ambapo Anna Mwakyusa amesema kituo kitawaepusha akina mama wajawazito kufuata huduma mbali na hivyo kupunguza hatari ya kupoteza maisha.
Theresia Paul, amesema huduma za mama na mtoto zitapunguza gharama kwa familia maskini ambazo zililazimika kugharamia usafiri kwenda Chamwino mjini.
Aidha amesema kituo hicho kitaleta unafuu mkubwa kwa wananchi wote, hasa kwa dharura za kiafya, na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha sekta ya afya nchini.






Social Plugin