
Na Bora Mustafa Fadhili - Arusha
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeendesha mafunzo maalum kwa waandishi wa habari jijini Arusha, ikiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Makamu Mwenyekiti wa Tume hiyo Mohamed Khamis Hamad amesema kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ni taasisi ya kiserikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyoanzishwa chini ya Ibara ya 129(1) ya Katiba ya mwaka 1977 inayojihusisha na kusikiliza malalamiko mbalimbali kuhusu uchaguzi, kufanya tafiti na kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa huru na haki.
"Tume ina jukumu la kuimarisha hifadhi ya haki za binadamu nchini na utawala bora pia inapokea na kuchunguza malalamiko yanayohusiana na uvunjifu wa haki hizo, kutoa elimu kwa umma, kutembelea vituo vya polisi na magereza, na kushauri serikali kuhusu mikataba ya kimataifa,” amesema Mohamed.
Aidha, amebainisha kuwa tume hiyo kwa sasa ipo katika mikoa 16 nchini, na moja ya malengo ya mafunzo hayo ni kufuatilia mwenendo wa kampeni hasa katika makundi maalum kama waandishi wa habari, ambao ni wadau muhimu wa utoaji wa taarifa kwa jamii.
Naye Afisa Uchunguzi Mkuu wa Tume, Mohamed A. Bakary, amesisitiza kuwa waandishi wa habari wana wajibu wa kuhabarisha umma, kufichua ukiukwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora, pamoja na kulinda haki hizo kupitia kazi zao.
Kwa upande wake mwandishi wa habari wa gazeti la Jamhuri Zulfa Mfinanga, mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa waandishi kwani yanawasaidia kuelewa vyema misingi, kanuni na maadili ya taaluma yao bila kuvunja haki za binadamu.
“Mwandishi anapoitumia taaluma yake kwa ufanisi, anaweza kujenga jamii, lakini akiitumia vibaya anaweza kuiharibu. Mafunzo haya yamekuja kwa wakati muafaka,” amesema Zulfa.
Social Plugin