Aliyekuwa mtia nia wa Ubunge Jimbo la Solwa, Mtaalamu wa Mipango na Usimamizi wa Maendeleo, Sosthenes Julius Katwale, amewataka wanachama na wananchi kuunga mkono wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Ametoa wito huo Septemba 15, 2025, wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM katika Jimbo la Solwa, kwenye mkutano uliofanyika Kata ya Lyamidati.
Katwale, ambaye ana uzoefu mkubwa katika masuala ya mipango, usimamizi wa ardhi, sera na maendeleo ya jamii, amesisitiza kuwa ni muda wa kuvunja makundi yaliyokuwa yamejitokeza kipindi cha kura za maoni na kushirikiana kuhakikisha ushindi wa CCM kuanzia ngazi ya Urais, Ubunge hadi Udiwani.
“Uchaguzi ndani ya chama ulishamalizika na mkutano mkuu kutuletea wagombea wa ubunge na udiwani. Hivyo ni muda wa kuungana pamoja kukipigania chama kupata ushindi katika nafasi zote yaani Rais, Mbunge na Madiwani. Ninamuombea kura Mgombea Urais Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mbunge wa Jimbo la Solwa Mhe. Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Itwangi Mhe. Azza Hillal Hamad na madiwani wote wa CCM. Nasistiza kuvunja makundi na kuwapa ushirikiano waliochaguliwa ili waweze kutuletea maendeleo,” amesema Katwale.Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Solwa kupitia CCM Ahmed Ally Salum, amewaomba wana CCM na wananchi kuvunja makundi yaliyokuwapo wakati wa kura za maoni na kuungana kwa lengo la kumtafutia kura Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na wagombea wote wa chama hicho.

“Hapa Lyamidati nasikia kuna makundi. Naombeni wana CCM wenzangu tuvunje makundi yote yaliyokuwapo kipindi cha kura za maoni, sababu wagombea wameshapatikana. Tuunganeni tusake kura CCM ishinde kwa kishindo. Kuendekeza makundi ni kujiumiza na kujipa presha bure,” amesema Ahmed.
Aidha, Ahmed ameahidi kuongeza kasi ya maendeleo katika Jimbo la Solwa, ikiwemo kumalizia tatizo la upatikanaji wa maji vijijini, ujenzi wa Zahanati na Vituo vya Afya, kuendeleza miundombinu ya barabara, pamoja na kushughulikia mgogoro wa hifadhi. Ameahidi pia kuanzisha mashindano ya michezo kwa vijana ili kuibua vipaji na kuwafungulia fursa za ajira.

Kwa upande wake, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal Hamad, amewaomba wananchi kumpa kura yeye pamoja na Rais Samia na Ahmed Ally Salum, akisema kufanya hivyo kutawawezesha viongozi hao kufanya kazi kama timu moja ya maendeleo.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Edward Ngelela, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kupiga kura na kuchagua “mafiga matatu” ya CCM, yaani Rais, Wabunge na Madiwani wote wa chama hicho.
Uchaguzi Mkuu utafanyika Oktoba 29, 2025 ambapo Watanzania watachagua Rais, Wabunge na Madiwani, huku kampeni zikiendelea katika maeneo mbalimbali nchini.


Social Plugin