Imeandaliwa na Dotto Kwilasa
Baada ya majina ya wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walioteuliwa kupeperusha bendera ya chama katika uchaguzi wa mwaka 2025 kutangazwa, jina la aliyekuwa Mbunge wa Tanga Mjini, Mhe. Ummy Mwalimu, halikuwemo.
Tofauti na ilivyo desturi katika siasa za Tanzania ambako mara nyingi kukatwa jina huambatana na maneno ya hasira, lawama, au malalamiko, kwa Ummy Mwalimu imekuwa tofauti ameonyesha kuwa siasa pia ni huduma, si nafasi tu ya madaraka.
Ametufundisha kuwa kukubali maamuzi kwa moyo wa shukrani kwa kujibu kwa busara na uadilifu, akionyesha kile wengi wanachokiita mfano wa kiongozi wa haki, mcha Mungu na mwenye maono ya kitaifa.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Ummy ameandika ujumbe mzito wa kutafakari, akianza kwa maneno yenye utulivu:"Mambo yote anapanga Mungu."
Kisha akaongeza kuwa Qur’an Tukufu imemfundisha kuupokea kila uamuzi kwa moyo wa shukrani, akiendelea kueleza kuwa amepokea maamuzi ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) kwa moyo wa kuridhika.
"Nitumie fursa hii kuwashukuru kwa kuniamini kuwa Mbunge wenu kwa kipindi cha miaka mitano (2020-2025),nafurahi kuona kuwa utumishi wangu kwenu umeacha alama za maendeleo."
Kauli hii imegusa nyoyo za wengi, ikizingatiwa kuwa Ummy Mwalimu amekuwa kiongozi mwenye ushawishi mkubwa, asiye na majivuno, mwenye kujali ustawi wa wananchi wake, hasa katika sekta ya afya, elimu, na uwezeshaji wa wanawake na vijana.
Akiwashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM Wilaya ya Tanga kwa kumpa kura nyingi kwenye mchakato wa kura za maoni, Ummy amesema,"Mlinikopesha imani kubwa sana,nitaienzi na kuithamini imani hii daima."
Akaongeza kuwa anaheshimu uamuzi wa vikao vya chama na akatoa pongezi kwa Kassim Mbaraka, ambaye ameteuliwa kupeperusha bendera ya CCM kwa Jimbo la Tanga Mjini.
Hakuishia hapo, bali ametoa wito wa mshikamano na ushirikiano,"Ninawaomba wanakimji wenzangu tumpokee na tumpe ushirikiano ili kuhakikisha ushindi pia unaenda kwa Rais wetu mpendwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan."amesema
Ummy Mwalimu ni Nani?
Mhe. Ummy Ally Mwalimu si jina geni katika siasa na uongozi wa Tanzania, ni kiongozi aliyejenga historia yake kwa utumishi wa umma uliojaa uwazi, weledi, na uchapakazi.
Ameshawahi kushika nyadhifa mbalimbali serikalini zikiwemo Waziri wa Afya (Katika vipindi tofauti),Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Mbunge wa Viti Maalum kabla ya kuwa Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kwa muda mrefu.
Katika nafasi zote hizo, Ummy amesimama kama mwanamke jasiri, msomi na mchapakazi, ambaye ameweka maslahi ya wananchi mbele kuliko maslahi binafsi.
Kwa wengi wanaomfahamu Ummy Mwalimu, huyu si tu mwanasiasa bali ni kiongozi anayejali, mwenye moyo wa kuhudumia watu, na ambaye amejijengea heshima kwa misingi ya kazi na sio maneno.
Historia yake katika utumishi wa umma ni pana na ya kuigwa.
Akiwa Waziri wa Afya katika vipindi tofauti, Ummy aliweka msisitizo mkubwa kwenye maboresho ya huduma za afya kwa mama na mtoto, uimarishaji wa vituo vya afya, na usambazaji wa vifaa tiba katika maeneo ya pembezoni.
Pia amewahi kuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ambako alisimamia ajenda ya kuwalinda watoto na kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Katika chama, Ummy ameheshimika kama mwanachama mtiifu na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kwa vipindi kadhaa na Uwepo wake ndani ya chama si wa kupita, bali umeacha alama kwa kuwa alijenga siasa za hoja, siasa za kujenga na siasa za kuheshimu taasisi.
Kauli zake baada ya kutopitishwa kwenye mchakato huu wa ubunge ni somo kubwa kwa viongozi wengine na jamii kwa ujumla.
Ametufundisha kuwa siasa si lazima iwe ya madaraka, bali ya kutumikia kwa muda uliopo, kwa bidii, heshima na uchapakazi.
Ametufundisha kuwa kiongozi wa kweli hujulikana si wakati wa mafanikio tu, bali pia katika namna anavyopokea changamoto na maamuzi magumu.
Kwa wakazi wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu ataendelea kubaki kwenye historia kama mmoja wa viongozi walioacha alama zisizofutika , alama za maendeleo, utu, upendo na uongozi wa haki.
Na kwa Tanzania nzima, ataendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa kizazi kijacho cha viongozi waadilifu

Social Plugin