Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RUZUKU YA MBOLEA YALETA MAPINDUZI YA KILIMO MADABA WAKULIMA WAMSHUKURU RAIS SAMIA

Baadhi ya wakulima wa mahindi kutoka Kijiji cha Mtyangimbole na wanachama wa Muungano wa Gumbiro Saccos wakichambua mahindi kwaajili ya kuuza kwa wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA 
Na Regina Ndumbaro-Madaba 

Wakulima wa mahindi kutoka Kijiji cha Mtyangimbole, Halmashauri ya Madaba mkoani Ruvuma, wameeleza furaha yao kwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka ruzuku kwenye mbolea ambayo imesaidia kupunguza gharama za uzalishaji. 

Bei ya mbolea sasa imepungua kutoka Shilingi 160,000 hadi 70,000 kwa mfumo mmoja wa kilo 25, hali iliyowezesha wakulima wengi kuongeza uzalishaji na kuhamasika kulima kwa tija. 

Wamesema hatua hiyo imerejesha matumaini kwa wakulima waliokuwa wamekata tamaa kutokana na gharama kubwa za kilimo.

Mkulima Wilgis Luambano amebainisha kuwa awali alikuwa akivuna gunia 10 hadi 15 tu kwa ekari moja, lakini baada ya kupata mbolea za ruzuku mavuno yameongezeka hadi gunia 25 kwa ekari. 

Mwanarabu Pili, mkulima mwingine wa kijiji hicho, ameeleza kuwa ruzuku hiyo imewasaidia wakulima wadogo ambao hapo awali walishindwa kumudu bei ya pembejeo, hivyo kumpongeza Rais Samia kwa uamuzi wa kuwapunguzia mzigo mkubwa wa kiuchumi.

Meneja wa SACCOS ya Muungano Gumbiro, Theoford Sefu, amesema chama hicho kimeongeza uzalishaji wake wa mahindi kutoka gunia 25 hadi 35 kwa ekari, kutokana na upatikanaji wa pembejeo za bei nafuu. 

Ameeleza kuwa msimu wa 2023/2024 waliweza kukusanya tani 350 za mahindi, huku matarajio ya msimu wa 2024/2025 yakiwa ni kukusanya tani 600. 

Ameongoza kuwa NFRA imefungua kituo cha ununuzi wa mahindi kijijini hapo, hali iliyosaidia wakulima kupata soko la uhakika na bei nzuri.

Mwenyekiti wa SACCOS hiyo, Elia Tenga, ameisifu Serikali kwa juhudi kubwa za kuwekeza kwenye kilimo, akisema katika kipindi cha miaka minne wameona mabadiliko makubwa katika maisha ya wakulima. 

Tenga amesema ruzuku ya mbolea imewawezesha wakulima wengi kujiunga na chama hicho na kupata mafanikio makubwa, huku akisema hakuna wakati wowote katika historia ambapo pembejeo zilikuwa nafuu kiasi hiki.Baadhi ya wakulima wa mahindi kutoka Kijiji cha Mtyangimbole na wanachama wa chama hicho cha Muungano wa Gumbiro Saccos wakichambua mahindi kwaajili ya kuuza kwa wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com