
Na Mwandishi Wetu - Malunde 1 blog
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa maagizo kwa viongozi wa Serikali kushiriki kikamilifu katika taratibu zote za mazishi ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali ya mgodi wa Nyandolwa, wilayani Shinyanga.
Akizungumza leo Agosti 22, 2025, katika eneo la tukio pamoja na viongozi wa Serikali na familia za waathirika, Lukuvi alisema Rais Samia amewatuma viongozi kuhakikisha kila msiba unahudhuriwa na Serikali kwa niaba yake, sambamba na kufikisha salamu za pole na rambirambi kwa wafiwa.
“Rais Samia kaniagiza kuwafikishia salamu za pole na rambirambi. Pia kanituma kuleta maagizo kwa viongozi waliopo hapa kuhakikisha wanahudhuria misiba yote ya watu waliopoteza maisha kwenye ajali hii na kuwasilisha rambirambi alizotoa,” alisema Lukuvi.
Ajali hiyo ilitokea Agosti 11, 2025, baada ya watu 25 kufukiwa na kifusi katika mgodi wa Kikundi cha Wachapakazi katika machimbo ya Nyandolwa.
Hadi sasa, watu 11 wametolewa, wakiwemo watatu waliookolewa wakiwa hai na nane wamefariki dunia, huku jitihada za kuwaokoa wengine 14 zikiendelea kwa kutumia mashine za kisasa za utambuzi wa ardhini.
Awali, Agosti 16, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, aliagiza kuanzishwa kwa ofisi ya muda ya mtendaji wa kijiji katika eneo la tukio ili kusajili wageni waliokusanyika wakisubiri taarifa za ndugu zao, ili waweze kuhudumiwa na Serikali.
Vilevile, Agosti 18, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, aliwataka wafiwa kuchagua wawakilishi wachache kati yao watakaobaki karibu na eneo la tukio ili kurahisisha uratibu wa huduma, akibainisha kuwa Serikali haitaki kuona familia zinapata changamoto za mahitaji muhimu wakati wakiwa kwenye huzuni.



Social Plugin