MABINGWA WA LIGI KUU SIMBA SC WATEKA BUNGE DODOMA...


Mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Tanzania bara (VPL) mwaka 2017/18, timu ya Simba leo wameliteka Bunge jijini Dodoma.


Mabingwa hao pamoja na benchi la ufundi na viongozi mbalimbali wa timu hiyo, wametembelea Bunge baada ya kupata mwaliko wa Spika Job Ndugai.


Hata kabla hawajatambulishwa na Mwenyekiti wa Bunge, Najma Giga, Naibu Waziri wa Tamisemi, Joseph Kakunda alianzisha 'shangwe' bungeni humo.


Ilikuwa hivi, kabla ya Kakunda kujibu swali la Mbunge wa Tabora Kaskazini (CCM), Almas Maige, Naibu Waziri huyo ameanza kwa kusema, leo Mei 14, 2018 ameamka saa 10 alfajiri kujiandaa kujibu maswali lakini kubwa ni furaha ya ubingwa.


Huku wabunge wakishangilia, Kakunda akiwa mwenye furaha akasema,"Sasa naamini Watanzania watapata wawakilishi wazuri wa michuano ya kimataifa, hawatatupa presha."


Kakunda muda wote wa kujibu maswali ya wabunge amekuwa akichombeza maneno ya furaha ya ubingwa wa Simba na uwapo wao bungeni.


Hakuwa Kakunda pekee, bali hata Mbunge wa Ilala (CCM), Azzan Zungu aliposimama kuuliza swali la kujua mikakati ya kuboresha michezo kwa vijana na akaanza kwa kusema:


"Humu ndani kaingia mnyama mkali sana, lakini tuko salama," na shangwe kuendelea ukumbini.


Mbunge wa Mpwapwa (CCM), George Lubereje naye kabla ya kuuliza swali amewapongeza Simba akisema wamefanya kazi kubwa sana kuchukua ubingwa hata kabla ligi haijaisha.
Na Ibrahim Yamola, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527