DR SLAA AFUNGUKA KUHUSU TRILIONI 1.5

Aliyewahi kuwa Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dkt. Wilbroad Slaa ambaye sasa ni Balozi wa Tanzania nchini Sweden amesema kuwa mjadala wa kuonekana au kutoonekana kwa sh 1.5 trilioni lililoibuka baada ya kuwasilishwa kwa Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) limetokana na udhaifu wa mfumo uliopo wa upitishaji wa bajeti.


Ameeleza kuwa hali hiyo inatokana na mfumo wa Bunge ambao unaruhusu wabunge kupitisha bajeti ambayo fedha zake hazipo tayari.


Dkt. Slaa amefafanua kuwa wabunge wamekuwa wakipitisha bajeti kabla ya fungu halisi kupatikana, ikiwa ni nadharia inayosubiri fungu hilo kupatikana kupitia kwa wafadhili au michakato mingine ya ukusanyaji.


“Kama fedha nyingi zinatumika bila kupitishwa na Bunge kwa sababu ndiyo mfumo wetu, unawezaje kuhoji fedha hizo zilitumikaje?” Dkt. Slaa anakaririwa na Mwananchi waliofanya naye mahojiano maalum.


Aliongeza kuwa kwa kawaida, huwezi kupata takwimu halisi za miradi mikubwa ya Serikali ndani ya kipindi cha mwaka wa fedha husika kwani miradi hiyo huwa katika hatua za utekelezaji.


Balozi Slaa ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Karatu kwa tiketi ya Chadema alisema kuwa kinachofanyika hivi sasa bungeni, wabunge wengi hawajadili hoja na badala yake wamekuwa watu wa kufanya ushabiki na kuhitimisha hoja tu.


Alisema kuwa wakati alipokuwa bungeni, alikuwa anafanya utafiti wa kutosha kuhusu masuala ya ufisadi na kuhakikisha anapata nyaraka zote husika kabla ya kuliwasilisha.


“Ndio maana unaona wakati huo niliweza kuwachachafya Mawaziri kwakuwa nilikuwa sikurupuki,” alisema.


Sakata la sh 1.5 trilioni liliibuliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe na baadaye kujibiwa na Serikali pamoja na Chama Cha Mapinduzi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527