ALICHOKIZUNGUMZA SUGU BAADA YA KUTOKA JELA

Saa chache baada ya kutoka jela, mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu Sugu amesema ni mfungwa wa kisiasa, “nilifungwa kiholela na nimetoka kiholela.”

Viongozi wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe leo Mei 10, 2018 walifika katika Gereza Kuu la Ruanda mkoani Mbeya kuwapokea Sugu na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga lakini walipigwa chenga ya mwili baada ya kuelezwa na askari magereza kwamba wameshatoka, hivyo kulazimika kuwafuata nyumbani. 

Akizungumza na MCL Digital leo Sugu amesema, “Sikutaka kuhoji sababu za kutolewa, jana niliambiwa jiandae kesho (leo) tutatoka, basi nasi tukasema haina shida kwa sababu sikuwa na sababu ya kuwa ndani. Naamini sikutakiwa kuwa gerezani.”

Sugu akiwa na Masonga alifika nyumbani kwake na kumkuta mlinzi pekee kutokana na mkewe Happiness Msonge kwenda Gereza la Ruanda kuwapokea.

Dakika chache baadaye Happiness na mke wa Masonga, Grace Malya walifika nyumbani hapo na kuwalaki kwa furaha huku wakikumbatiana na kucheka.

Akizungumzia mazingira ya kuachiwa kwa wawili hao, Mbowe amesema, “inaonyesha hawakuwa na sababu ya kuwepo gerezani maana mazingira ya kutolewa kwao ni tata sana.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527