KUHUSU TOFAUTI YA MASOGANGE ALIYEKUWA HAI NA MASOGANGE MAREHEMU

Agnes Gerald halikuwa jina maarufu sana. Wengi walimfahamu kwa jina la Masogange. Mbali na kupata umaarufu kwa kupamba video za wasanii, ujio wa mtandao wa Instagram ulilikuza jina lake. Ukitafuta jina Masogange katika mtandao huo zinakuja kurasa zaidi ya 50 zote zikiwa zimesheheni wafuasi wa kutosha.


Umbile lake zuri lilipamba kurasa hizo ingawa miongoni mwa wengi alionekana mwanamke asiye na maadili. Wapo ambao hawakupendezwa na mavazi yake na namna alivyoanika maungo yake.


Kwa wengine alikuwa mtoto, mama, dada, rafiki na ndugu tegemezi lakini bahati mbaya upande wake huu mwingine umekuja kujulikana akiwa ametangulia mbele za haki.


Mwanasiasa Julius Mtatiro aliandika makala ndefu akieleza namna ambavyo Masogange hakutendewa haki wakati akiwahi hai. Kifo chake kinajenga taswira za maisha ya ndani ya vijana wengi wa Taifa letu.


Taswira ya kutwishwa mizigo mizito wakiwa wadogo, kuharibiwa, kutelekezwa, kujitafutia maisha, kuonyesha vipaji vyao na vipaji hivyo kutumiwa na watu wengine kwa manufaa ya watu hao huku vijana wetu wakibaki na taswira hasi na kuonekana wavunja maadili.


Mbali na kuonekana asiye na maadili, kesi ya kusafirisha dawa za kulevya na kutumia ni miongoni mwa yaliyomchafua.


Huenda leo hadithi zingebaki kuwa nyumba ya hadhi ya kawaida kabisa ya baba yake lakini ushujaa wake unathibitika kwamba pamoja na sifa mbaya alizopewa, alikuwa binti mwenye huruma aliyekumbuka ndugu zake ikiwamo kumjengea nyumba baba yake.


Wasanii wenzake wanamlilia kila mmoja akimzungumzia namna alivyokuwa nje ya umaarufu wake. Belle 9 ambaye alimtumia katika wimbo uliompa jina hilo takriban miaka minane iliyopita, anamlilia akikumbuka mazuri mengi ya binti huyo.


Irene Uwoya ambaye amediriki kuchora tattoo ya binti huyo anasema hatatokea rafiki wa kweli kama Masogane.


Kwa ndugu zake ni mkombozi wa familia. Dada zake wanalia kwamba nguzo ya familia imeanguka. Alikuwa akisomesha watoto wa ndugu zake na kuwahudumia kwa mahitaji mengine. Muhimili wa familia yao umeanguka.


Chanzo- Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527