WANANCHI WAVAMIA KITUO CHA POLISI..WATELEKEZA MWILI WA MAREHEMU KWENYE KITANDA CHA MWENYEKITI WA MTAA GEITA

Baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Nyakabale wilayani Geita wametelekeza mwili wa marehemu nyumbani kwa mwenyekiti wa mtaa huo, Elias Ndarawa.

Ndarawa anatuhumiwa kutoshughulikia tukio la Zacharia Shaban kupigwa na polisi jamii hadi kufa.

Wananchi hao waliubeba mwili wa Zacharia na kuulaza kwenye kitanda cha mwenyekiti huyo.

Majaliwa Shaban ambaye ni ndugu wa marehemu Zacharia amesema leo Machi 12,2018 kwamba nduguye alipigwa Machi 5,2018 akiwa eneo la Mgodi wa Dhahabu Geita (GGM) akiokota mabaki ya mawe ya dhahabu maarufu magwangala.

Amesema Zacharia alipelekwa polisi alikokaa kwa siku sita na aliporudi uraiani hali yake ilikuwa mbaya.

Majaliwa amesema nduguye alipelekwa hospitali alikofariki dunia Jumamosi Machi 10,2018 na hadi sasa hakuna kiongozi aliyefika kwenye msiba huo wala kutoa kauli yoyote.

Mkazi wa mtaa huo, Johnson John amesema hawapo tayari kuzika hadi Serikali itakapotoa kauli kuhusu hatima ya maisha yao kwa kuwa polisi jamii wamekuwa wakiwapiga na kuwajeruhi.

Jana, Machi 11,2018 wananchi walivamia eneo la kituo cha polisi jamii kilichopo mtaa wa Manga na kukichoma moto kwa madai kwamba wamempiga na kumuua Zacharia.

Na Rehema Matowo, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527