POLISI : NONDO ALIKWENDA KWA MPENZI WAKE ...."ALIJITEKA MWENYEWE KUTAFUTA UMAARUF WA KISIASA"


 Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na polisi mkoani Iringa limebaini na kujiridhisha kuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo hakutekwa, bali ‘alijiteka’ mwenyewe.

Akizungumza leo Jumanne Machi 13, 2018 kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema polisi watachukua hatua za kisheria kwa kuwa mwanafunzi huyo amewadanganya watu kuwa ametekwa na kusababisha taharuki kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.

Mambosasa amesema polisi wamefanya uchunguzi na kubaini mwanafunzi huyo hakutekwa bali ‘alijiteka’ mwenyewe ili kutafuta umaarufu wa kisiasa na kusababisha kuzua tafrani kwa jamii.

Amesema Machi 6, 2018 saa sita usiku zilisambaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Nondo ametekwa na watu wasiojulikana.

Amebainisha kuwa polisi wa kdana hiyo walianza kufuatilia ili kubaini ukweli wa tukio hilo ikiwa pamoja na kufunguliwa jalada la uchunguzi lenye kumbukumbu namba DSM/KIN/CID/P.E/51/2018.

Mambosasa amesema Machi 7, 2018 walipewa taarifa na polisi mkoani Iringa kuwa mwanafunzi huyo ameonekana Wilaya ya Mafinga akiwa na afya njema na mwenye kujitambua akiendelea na shughuli zake.

“Mwanafunzi huyu alionekana Mafinga akiendelea na shughuli zake na wala hakuripoti tukio la kutekwa katika kituo chochote cha polisi hivyo tunaendelea kumshilikia hivyo taratibu ili tumpeleke mahakamani,”amesema Mambosasa.

Amesema upelelezi umebaini mwanafunzi huyo alikwenda kwa mpenzi wake ambaye alikuwa akifanya naye mawasiliano mara kwa mara akiwa njiani kuelekea Iringa. 

"Pengine alitaka kuzua hilo ili kujipatia umaarufu ila upelelezi uliendelea kubaini kuwa mwanafunzi huyo alikwenda Iringa kwa mpenzi wake ambaye alikuwa akiwasiliana naye mara kwa mara akiwa njiani kuelekea Iringa hii ni baada ya kufanya uchunguzi wa kisayansi na kubaini muda ule aliosema ametekwa simu yake imeendelea kuonyesha mawasiliano aliyokuwa anafanya na huyo binti ambaye alikuwa amemfuata" ,alieleza Mambosasa. 

Mambosasa amesema kuwa walipomkamata walikuwa na mashaka kuwa huenda akawa amepatwa na ugonjwa wa malaria ya kichwa iliyopelekea kufanya hayo na kudai kuwa alipelekwa hospitali na kupimwa na kuonekana kuwa mzima asiye na matatizo yoyote ya kiakili. 

"Alikuwa ni mzima wa afya njema na haya aliyafanya kwa makusudi kwa sababu anazozijua yeye mwenyewe, jeshi la polisi limebaini kuwa mwanafunzi huyo alikuwa huru baada ya kutoka Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, alisafiri akiwa huru na akafika Iringa akiwa salama, kwa hiyo ni uzushi mtupu uliokuwa na malengo ya hovyo lakini kuna watu wengine walilishabikia jambo hili wengine huwezi kuamini kwa nafasi zao walilishabikia jambo hili la hovyo mtu kujizushia jambo"alisema Mambosasa 

Nondo alidaiwa kutoweka Machi 6, 2018 lakini alijisalimisha mikononi mwa polisi wilayani Mafinga, Iringa Machi 7. 

Baada ya kujisalimisha alifunguliwa jalada la uchunguzi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire ambaye aliwaeleza wanahabari kuwa uchunguzi huo unalenga kubaini iwapo ni kweli alitekwa au alitoa taarifa za uongo kwa lengo la kuhamasisha wanafunzi kuvuruga amani. 

Machi 10, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda aliliomba Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa litakapomalizana na Nondo limrejeshe jijini Dar es Salaam ili na yeye aanzishe uchunguzi wake kwa mwanafunzi huyo. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527