POLEPOLE : WASIMAMIZI NA WARATIBU TASAF SHIRIKIANENI NA VIONGOZI WA VIJIJI KUBUNI MIRADI KUSAIDIA KATA MASKINI BADALA YA KUWAPA PESA TU


KATIBU wa itikadi na uenezi wa Chama cha Mapinduzi Taifa, Humphrey Polepole amewashauri wasimamizi na waratibu wa Mpango wa kunusuru Kaya Masikini -TASAF kushirikiana na viongozi wa vijiji na wataalamu wa ardhi kuanzisha miradi itakayokuwa endelevu na itakayowaondoa haraka wanufaika wa mfuko katika umaskini badala ya kuwapatia pesa pekee.

Alitoa ushauri jana akiwa katika ziara yake ya kutembelea wanufaika wa mfuko huo wa maendeleo wilayani Kibondo katika kijiji cha Nyabitaka kata ya Kizazi wilayani humo mkoani Kigoma.

Akiwa katika kijiji hicho,Polepole alikagua Shamba darasa lenye hekari mbili la kilimo cha mseto cha kulima mazao mchanganyiko kinachosimamiwa na wanufaika hao,alisema lengo la serikali ni kuwaondoa wananchi katika umaskini unapompatia fedha haziwezi kumsaidia kuondoka kwenye umaskini haraka.

Alisema kilimo cha karanga ni kilimo kinachochukua muda mfupi kukomaa na kinaweza kuwaondoa haraka wanufaika hao kwenye umaskini, akidai wataalamu wameeleza na baadhi ya wanufaika kulima hekali moja wanapata gunia 90 sawa na shilingi 900,000/=.

Polepole alishauri waratibu wa mfuko wa maendeleo kushirikiana na wataalamu wa ardhi na viongozi wa vijiji kutenga matumizi bora ya ardhi na kutenga mashamba kwa ajili ya wanufaika badala ya kuwapatia shilingi elfu 40,000/= kwa kila mwezi watenge kilimo wakisimamie wanufaika hao baada ya mwaka mmoja wanafaika hao hawatakuwa na umaskini tena na wataendele kujikwamua kwa kilimo hicho wao wenyewe.

"Serikali ya CCM imeandaa mpango huu wa maendeleo, mpango kwa ajili ya kunusuru kaya maskini na lengo likiwa ni kuwainua watu watoke kwenye umaskini uliopitiliza na watu watoke kwenye unyonge,wapate fedha na wawe na miradi endelevu huo ndiyo mpango wa serikali... unapompatia mnufaika fedha haimsaidii kuondoka kwenye umaskini lazima uitumie fedha hiyo kubuni miradi itakayowaondoa wananchi moja kwa moja katika umaskini",alieleza.

Alisema mwaka 2025 mpango huo wa TASAF utakwisha endapo utamalizika na wananchi hawajapatiwa miradi ya kujikwamua na umaskini watakuwa hawajawasaidia chochote.

Pia alitembelea shamba la miti la wanufaika katika kijiji cha Mkalazi kata ya Mabamba na kukuta wanufaika wamepanda miche ya mbao 49000 na kuagiza miti hiyo iwe mali ya wanufaika na serikali ya kijiji itafute eneo lake ipande miti na watakapo wanyang'anya wanufaika watakuwa hawajawasaidia.

Aidha Polepole aliahidi wananchi wilayani Kibondo kuwa serikali ya awamu ya tano ya CCM itatoa kiasi cha shilingi milioni 52 kwa ajili ya wananchi wakopeshwe na waweze kuondoka katika umaskini na kuwaomba watendaji na wenyeviti wa vijiji kuandaa utaratibu bora wa kuwakopesha wananchi hao kwa utaratibu mzuri.

Nae Mratibu wa mfuko wa maendeleo wa kunusuru kaya maskini TASAF mkoani Kigoma Jailos Pilla alisema utaratibu wa mfuko huo ni kwamba wanufaika wanabuni mradi ambao wanakuwa wanafanya kazi baada ya kufanya kazi wanausimamia na kila siku wanalipwa shilingi 2300/= na baada ya hapo mradi huo unakuwa ni mali ya serikali ya kijiji na wanufaika hawausiki na miradi hiyo tena.

Alisema kila mnufaika anatakiwa kujifunza kupitia miradi hiyo inayoanzishwa ili aweze kuanzisha nyumbani kwake ili kuweza kujikwamua katika umaskini na wanufaika wengi wamefanya hivyo na mpaka sasa wapo wengi wamejenga nyumba za bati na wanasomesha kupitia fedha za TASAF walizopatiwa na kubuni miradi yao binafsi.

Kwa upande wake Lucia Mihayo ambaye ni mnufaika wa mfuko wa TASAF alisema fedha alizozipata alizitumia kununa tofali na bati na mpaka sasa ameanza ujenzi wa nyumba ya bati ili aweze kuishi vizuri na watoto wake na ameanzisha mradi wa kufuga mbuzi aweze kusomesha watoto wake.

Naye Elizabeth Ndambulo alisema alipopatiwa fedha hizo alilima karanga na baada ya kulima hekari mbili alivuna na akauza akapata fedha ya kujenga nyumba na kuwalea watoto wake mpaka sasa ameanza kuona maisha yake yakinadilika kutoka katika hali ya chini aliyokuwa nayo na kuwa na hali nzuri ya kiuchumi tofauti na mwanzo.

Hata hivyo polepole amewatembelea wanufaika wa mfuko wa maendeleo wa kunusulu kaya masikini Wilayani Kibondo pamoja na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo kikiwemo kituo cha Afya cha Mabamba na kuwapongeza kwa ubunifu walioufanya kutumia fedha kidogo kukamilisha jengo hilo kwamba wametekeleza vizuri sera ya chama cha mapinduzi na kushiriki katika ujenzi wa msingi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari Lubanga kata ya Rusohoko wilayani humo.

Na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog
Katibu wa itikadi na uenezi wa Chama cha Mapinduzi Taifa, Humphrey Polepole akizungumza kijiji cha Nyabitaka kata ya Kizazi wilayani humo mkoani Kigoma- Picha zote na Rhoda Ezekiel - Malunde1 blog



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527