MAHAKAMA YAPOKEA RUFAA YA MBUNGE SUGU NA MASONGA

Rufaa ya kupinga hukumu ya kifungo cha miezi mitano jela iliyotolewa kwa mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga imewasilishwa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya.


Akizungumza leo Machi 1, 2018 mmoja wa mawakili wa Sugu, Faraji Mangula amesema tayari maombi ya rufaa yao yamepokewa leo mchana na kupewa kumbukumbu namba 29/2018.


“Tayari rufaa yetu imeshapokewa Mahakama Kuu (Mbeya) na tunachosubiri ni kupangiwa tarehe ya kuanza kusikiliza tu, ila tunachoshukuru watu wa Mahakama hii wapo vizuri kushughulikia suala hili,” amesema Mangula.


Mbali na kukata rufaa hiyo, lakini pia mawakili hao wanakusudia kuomba dhamana kwa wateja wao ili waweze kuwa nje katika kipindi ambacho wanakuwa wanasikiliza rufaa yao.


Sugu na Masonga walihukumiwa baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.


Wawili hao walitoa kauli hiyo Desemba 30 mwaka jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527