DIWANI WA CCM MBARONI KWA KUMPIGA NGUMI ZA USO MUUGUZI WA KITUO CHA AFYA BUNAMBIU SHINYANGA


Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule
***

Jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga linamshikilia diwani wa kata ya Bunambiu wilayani Kishapu Richard Sangisangi(48) kupitia Chama Cha Mapinduzi kwa kumshambulia kwa kumpiga ngumi usoni na kifuani muuguzi wa kituo cha afya Bunambiu Hilda Simon (35). 

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari leo,Machi 9,2018 Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Simon Haule alisema Sangisangi alimpiga muuguzi huyo katika kituo cha afya Bunambiu na kumsababishia maumivu makali. 

Alisema chanzo cha tukio hilo lililotokea Machi 8,2018 majira ya saa tatu na nusu asubuhi ni diwani huyo kutokuwa na na imani na muuguzi huyo wakati akiwahudumia wagonjwa hivyo kuamua kumshambulia kwa kumpiga ngumi. 

“Mtuhumiwa tumemkamata na tutamfikisha mahakamani mara tu baada ya taratibu za kiupelelezi kukamilika,natoa wito kwa wananchi na viongozi kuacha kujichukulia sheria mkononi”,alisema kamanda Haule. 

Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo,waliiambia Malunde1 blog kuwa diwani huyo alimtuhumu muuguzi huyo kuwa hahudumii wagonjwa vizuri na kumtaka aondoke kituoni na alipogoma ndipo diwani alipoamua kumshambulia mbele ya wagonjwa. 

Walisema diwani huyo alipigiwa simu na wananchi wakimwelezea kuwa mgonjwa wao aliyelazwa katika kituo hicho cha afya hapatiwi huduma vizuri na ndipo diwani huyo alipoomba kuongea kwa simu na muuguzi wa zamu,muuguzi akamsihi diwani afike kituoni na alipofika akaanza kumshambulia muuguzi huyo. 

“Huyu diwani alipigiwa simu na ndugu wa mgonjwa,kwamba mgonjwa wao hapatiwi huduma vizuri hali inayosababisha aendelee kulazwa”,walieleza. 

Hata hivyo habari zaidi zinasema,wakati Hilda Simon akiendelea kuhudumia wagonjwa,ghafla muuguzi mwingine ambaye hakuwa zamu aliingia katika wodi ya wagonjwa na kuwaambia ndugu wa mgonjwa huyo kuwa ndugu yao ana upungufu wa damu hivyo anatakiwa kupewa rufaa kwenda hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga. 

“Kutokana na hali hiyo ndipo ndugu wa mgonjwa wakaamua kumpigia simu diwani na kutaka kuongea kwa simu na nesi wa zamu,nesi akaomba diwani afike ofisini,alipofika ndipo akaanza kuonesha ubabe kwa kumshambulia muuguzi ambaye alikuwa zamu na alikuwa anasimamia kituo cha afya kutokana na mganga mkuu wa kituo kutokuwepo kazini”,walisema mashuhuda wa tukio hilo. 

Tukio hilo limetokea wakati wanawake wakisherehekea  siku ya wanawake duniani.

Na Kadama Malunde- Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527