ZITTO KABWE ATEMA CHECHE SHINYANGA..."NCHI HAIWEZI KUWA YA CHAMA KIMOJA LICHA YA NGUVU NYINGI KUUA UPINZANI"

Kiongozi wa chama cha Act Wazalendo Taifa Zitto Kabwe, 
amewataka wanachama wa ACT Wazalendo kutotereka na hali ya siasa ambayo kuna ubinywaji wa demokrasia na kusisitiza kuwa nchi hii haiwezi kurudi kwenye mfumo wa chama kimoja licha ya nguvu nyingi kutumika ya kuua upinzani.

Alisema kinachopaswa kufanyika ni kusimama imara na kupigania demokrasia ya kweli ambayo itawafanya watu kuwa huru na kufanya kile wanachokitaka bila ya kuvunja sheria za nchi.

Zitto ameyasema hayo leo Februari 28 mjini Shinyanga akiwa kwenye ziara yake ya kuimarisha chama alipokutana kuzungumza na viongozi pamoja na wanachama wa chama hicho mjini humo, na kuwataka wasitetereke na uendeshwaji wa siasa hapa nchini na kuanza kuhama vyama hovyo bali wajipange kisaikolojia na kukijenga chama.

Alisema siasa za sasa  nchini Tanzania ni ngumu, hivyo wasikate tamaa kuendeleza mapambano ya kupigania demokrasia hapa nchini, pamoja na kuendelea kuulinda mfumo wa vyama vingi ambao ndiyo mkombozi kwa watanzania na waendelee kujipanga kugombea majimbo katika chaguzi hizo ukiwemo  uchaguzo mkuu wa mwaka 2020.

Zitto Kabwe alieleza kuwa kutokana na jambo hilo la kubinywa kwa demokrasia hapa nchini wanapaswa kujiandaa kisaikolojia kwenye chaguzi hizo na kutotishika na watu wanaohama vyama vya siasa, bali waanze kujipanga mapema namna ya kulinda wizi wa kura, kutafuta mawakala waaminifu pamoja na viongozi kutatua kero za wananchi.


“Tunataka chama chetu kiwe tofauti na vyama vingine vya upinzani kwa kutohama hama vyama kwa kuhofia uchaguzi mkuu ujao kuwa hawatopata kura wala uongozi, bali sisi tujipange kisaikolojia na kufanya kazi ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi, ambao ndio wenye ridhaa ya kutupatia uongozi,”alisema.

Aliwataka viongozi wa chama hicho ambao walipewa ridhaa ya wananchi kwenye chaguzi zilizopita (2014-15) za serikali za mita,madiwani na ubunge wawatumikie wananchi ipasavyo kwa kutatua kero zao ili kuonyesha utofauti wa viongozi wa ACT na wa vyama vingine ili kuendelea kukiimarisha chama kwa wananchi.

Nao baadhi ya wanachama hao akiwemo Maarufu Hassani, walionyesha wasiwasi juu ya baadhi ya viongozi ambao walipata ridhaa kwenye chaguzi zilizopita (2014-15) kuwa kutokana na vuguvugu la kisiasa hapa nchini la kubinywa kwa demokrasia na chaguzi zinavyoendeshwa kuwa kuna uwezekano wa viongozi hao wasirudi 2020.

Katika ziara hiyo, Zitto alifanikiwa kuvuna wanachama wapya Tisa kutoka vyama mbalimbali vya siasa ambapo aliwapatia kiapo cha utii wa chama hicho ili kuendelea kukilinda na kukijenga chama kwa wananchi ambao ndio watawapatia ridhaa ya kushika nchi.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Zitto Kabwe ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Kigoma mjini akizungumza na wafuasi wa chama cha ACT Wazalendo leo mjini Shinyanga- Picha zote na Marco Maduhu - Shinyanga News & Malunde1 blog
Awali Katibu wa Jimbo wa chama cha ACT Wazalendo mjini Shinyanga Merkyoli Tafuta akimkaribisha kiongozi huyo wa kitaifa Zitto Kabwe pamoja na kuwatambulisha viongozi mbalimbali wa chama hicho mkoani Shinyanga na baadhi ya wanachama ambao walihudhuria kikao cha kiongozi huyo ambacho kililenga kuimarisha chama.
Mjumbe wa Kamati kuu ya Chama hicho Taifa Nyangaki Shilungushela,akizungumza kwenye kikao hicho ambapo aliwataka wanachama hao wa ACT Wazalendo kuendelea kujiamini na kufanya kazi licha ya chama chao kubezwa kuwa ni kichanga na CCM "B" bali wao wasiangalie propaganda za wakosaji ikiwa chama hicho kwa sasa ndiyo mpinzani wa kweli na ndio kina aminiwa na wananchi katika kuwaletea ukombozi.
Wanachama wa ACT Wazalendo wakiwa kwenye kikao cha kiongozi wao wa chama hicho Taifa Zitto Kabwe, na kuaswa kuendelea kukijenga chama na kutotetereka na siasa za ubinywaji wa demokrasia ambazo zinaendeshwa hapa nchini.
Wanachama wa ACT Wazalendo wakiendelea na kikao cha kiongozi wao wa kitaifa Zitto Kabwe.
Wanachama wa ACT Wazalendo wakiwa kwenye kikao wakisikiliza ujumbe mbalimbali kutoka kwa kiongozi wao wa chama hicho taifa Zitto Kabwe.
Kikao kikiendelea.
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo mkoa wa Shinyanga Siri Yasini, akimkaribisha kiongozi wa chama hicho Taifa Zuberi Zitto Kabwe, kupokea wanachama wapya tisa ambao wamejiunga na chama kutoka vyama mbalimbali vya siasa.
Kiongozi wa chama hicho Taifa Zitto Kabwe, akimpatia kadi ya chama hicho Mwanachama mpya Ester Mtupili ambaye alikuwa mwanachama wa Chadema.
Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe akiongoza kiapo cha utii wanachama wapya tisa waliojiunga na chama hicho wakitokea vyama mbalimbali vya kisiasa.
Zitto Kabwe akiwataka wanachama wapya na wazamani kuungana kwa pamoja kukijenga chama, na kuachana na siasa za malumbano, bali wajikite kukipigania chama ili kuendelea kuaminiwa na wananchi ambao ndio wenye ridhaa ya kuwapatia viongozi wengi kwenye chaguzi zijazo ukiwamo uchaguzi mkuu 2020, kwa kuwapatia madiwani wengi ,wenyeviti, na wabunge na hata kushika dola.
Wanachama wa ACT Wazalendo wakipiga picha ya pamoja na kiongozi wao wa chama hicho Taifa Zitto Kabwe.

PICHA KWA HISANI YA SHINYANGA NEWS BLOG

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527