WAZIRI MPINA AKAMATA MELI YA UVUVI HARAMU NA KUITOZA FAINI YA MILIONI MIA SABA SABIN


Waziri wa Mifugo  na Uvuvi Luhaga Mpina akiangalia mzigo wa mapezi ya samaki aina ya papa wakati Kapteni Han Ming Chuan wa Meli ya Buah Naga 1 akifungua mfuko wenye Mapezi yaliyokamatwa kinyume na Sheria ya Usimamizi  wa Bahari Kuu(DSFA) ya Mwaka 1998 kama ilivyorekebishwa Mwaka
2007.Meli hiyo ilitozwa faini ya shilingi milioni 770. Picha na John
Mapepele
Waziri wa Mifugo  na Uvuvi Luhaga Mpina akiangalia pezi la samaki aina ya papa wakati alipokagua Meli ya Buah Naga 1 yenye Mapezi yaliyokamatwa kinyume na  Sheria yaUsimamizi wa Bahari Kuu (DSFA) ya Mwaka 1998 kama ilivyorekebishwa Mwaka 2007.
Waziri wa Mifugo  na Uvuvi Luhaga Mpina akitoka kwenye Meli ya Buah Naga 1 baada ya kuikagua ambapo ilikutwa na mapezi ya samaki aina ya papa kinyume na Sheria ya Usimamizi wa Bahari Kuu(DSFA) ya Mwaka 1998 kama ilivyorekebishwa Mwaka 2007.
Meli ya Buah Naga 1 iliyokamatwa eneo la Mtwara ikiwa na kilo 90 ya mapezi ya samaki aina ya papa yaliyokamatwa kinyume na Sheria 

***
Waziri wa Mifugo  na Uvuvi Luhaga Mpina ameridhia utozwaji wa faini ya dola za Kimarekani laki tatu na nusu sawa na shilingi milioni mia saba na sabini iliyotozwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu (DSFA) kwa Meli ya Buah Naga 1 kutoka nchini Malaysia kwa kosa la kukutwa  mapezi ya samaki aina ya papa kilo 90 huku miili ya samaki hao kutupwa baharini kinyume na kanuni ya 66 ya kanuni za bahari kuu za mwaka 2009 na kifungu namba 18(2) cha Sheria yaUsimamizi  wa Bahari Kuu(DSFA) ya Mwaka 1998 kama ilivyorekebishwa Mwaka 2007.

Akizungumza  baada ya kukagua meli hiyo leo mjini Mtwara, Waziri Mpina alisema kuwa  wamiliki wa meli hiyo wanatakiwa kulipa faini hiyo ndani ya siku saba ambapo kama hawatalipwa watapelekwa mahakamani mara moja na kushtakiwa
kwa mujibu wa sheria za nchi.

Aidha Mpina amesema Serikali imetaifisha tani nne na nusu za samaki ambazo zitauzwa mara moja kwa njia ya mnada na kwa kuzingatia taratibu mbalimbali za serikali.

Akitoa taarifa ya kukamatwa kwa meli hiyo, kwa Waziri, Kiongozi wa Kikosi Kazi maalum cha kudhibiti uvuvi haramu, Kamishna Frederick Milanzi wa Tume ya Kupambana na Madawa ya Kulevya nchini amesema kwamba Kapteni wa meli hiyo Han Ming Chuan raia wa Malaysia alikutwa na bastola aina
ya Bereta na risasi kumi ambayo alikuwa anaimiliki kinyume cha
sheria.

Amesema kuvua na kutupa mizoga ya samaki baharini siyo tu kwamba wanahujumu raslimali za uvuvi baharini bali pia wanachangia katika uchafuzi wa mazingira ya baharini.

Pia Waziri Mpina amesisitiza kuwa Serikali haipo tayari kufanya kazi na wawekezaji wababaishaji  kwenye sekta ya uvuvi na kwamba kuanzia sasa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayejaribu kuhujumu raslimali za uvuvi
na kujihusisha na uvuvi haramu.

Aidha Waziri Mpina  ametoa onyo kali kwa wawekezaji wa uvuvi kwenye bahari ya Tanzania kuacha kutumia mwanya wa kupewa kibali cha kuvua na kujihusisha na makosa mbalimbali.

Ameyataja baadhi ya makosa hayo kuwa ni pamoja na usafirishaji haramu wa silaha, binadamu, madawa ya kulevya na nyara za serikali ikiwemo meno ya tembo.

Pia usafirishaji wa mazao ya misitu na samaki.

Kwa upande wake, Bw. Wankyo Simon ambaye ni Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Divisheni ya Mashtaka Makao Makuu Dar es Salaam na Mkuu wa Dawati linalohusiana na Makosa ya Mazingira, amesema makosa
ya namna hii ni makubwa na endapo kiwango hicho cha pesa hakitalipwa kama ilivyoamriwa, taratibu za kiupelelezi zitakamilishwa na kapteni wa Meli hiyo atafikishwa mahakamani kwa makosa yaliyoainishwa ambapo anaweza kupewa adhabu ya kifungo na meli hiyo kutaifishwa na kuwa mali
ya Serikali. 

Pia amependekeza kuwepo kwa mwongozo wa uendeshaji mashauri (Standard Operating Procedures) kwa makosa yanayofanyika baharini ili uweze kutumiwa na wadau mbali mbali kuanzia ukamataji wa chombo husika, upelelezi wake, namna bora
ya kutunza chombo hicho na uendeshaji wa mashauri yanayotokana na operesheni zote zinazofanyika baharini. 

Alisema mwongozo utasaidia kuimarisha kesi zote zinazoenda mahakamani kuanzia inapofunguliwa mpaka kufikishwa mahakamani na wadau wote watajua kwa urahisi namna ya kusimamia utekelezaji wa majukumu yao.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa (DSFA) Hosea Mbilinyi amesema Mamlaka yake imegundua kuwepo kwa  baadhi ya wawekezaji wasiofuata taratibu na Sheria za kufanya shughuli za uvuvi katika bahari ya Tanzana ambapo amesema tayari Mamlaka imeshawapiga faini ya dola za kimarekani laki moja kwa meli tatu zilizofanya makosa katika sikuza hivi karibuni.

Katika siku za hivi karibuni Waziri wa Mifugo na Uvuvi ameunda timu iliyoshirikisha  wataalam kutoka katika vyombo mbali vya Serikali kuendesha operesheni maalum ya kutokomeza uvuvi haramu nchini ambayo licha ya kupata mafanikio makubwa imetoa hamasa kwa wavuvi kuanza kusalimisha  zana haramu za uvuvi na kuziteketeza.

Na John Mapepele, Mtwara

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527