WATUMISHI WALIOONDOLEWA KAZINI KWA VYETI FEKI HAWANA MADAI YOYOTE SERIKALINI




Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma na Utawala Bora imesema watumishi wote waliondolewa katika utumishi wa umma kwa sababu ya kukosa vyeti vya kidato cha nne hawana madai yoyote Serikalini.


Kauli hiyo imetolewa leo, Februari 12, 2018 na Kaimu Katibu Mkuu katika ofisi hiyo, Mathias Kabunduguru katika kikao cha wakurugenzi wa utawala na rasilimali watu wa wizara zote, makatibu tawala, wasaidizi mkoa na wakuu wa idara za utumishi na utawala.


Amesema zoezi la uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa umma lilihitimishwa Oktoba, 2017 na wale wasiokuwa na vyeti vya kidato cha nne waliambiwa waondoke kwa hiari yao.


Hata hivyo, amesema bado watumishi wasio na vyeti hivyo wako kazini kama ilivyobainika katika Wilaya ya Kwimba.


Amewataka maofisa utumishi kuwaondoa wale waliobakiwa kwa sababu watakapowagundua wataadhibiwa wao na wakurugenzi wao.


"Muwaondoe wote katika orodha ya watumishi wa umma na katika orodha ya mishahara na watakaondolewa wote hawana madai yoyote Serikalini," amesema.


Amesema watafanya ukaguzi wa kushtukiza kukagua watumishi wasio na vyeti hivyo katika ofisi za umma ili kujiridhisha.


Watumishi hao waliokosa sifa pamoja na wale waliobainika kuwa na vyeti bandia waliagizwa kujiondoa wenyewe kwenye utumishi wa umma mwaka 2016, ambapo Rais John Magufuli alianzisha ‘vita’ dhidi ya wafanyakazi waliokosa sifa ambao walikuwa serikalini.


Na Sharon Sauwa, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527