Picha : AGAPE NA POLISI WAKUTANA NA WANAFUNZI WA SHULE YA MSINGI UJAMAA NA MWAMALILI SEKONDARI


Meneja mradi wa kuzuia mimba na ndoa za utotoni kutoka Shirika la AGAPE Mustapha Isabuda akitoa elimu kwa wanafunzi wa shule ya msingi Ujamaa iliyopo katika kijiji cha Seseko kata ya Mwamalili Manispaa ya Shinyanga kupaza sauti pale wanapofanyiwa vitendo vya ukatili. Aliwataka kutokaa kimya bali watoe taarifa kwa walimu,wazazi ama viongozi wa serikali ili vitendo hivyo vikome na wanafunzi wapate kutimiza ndoto zao - Picha na Marco Maduhu- Malunde1 blog 
Mkurugenzi wa Shirika la AGAPE John Myola akitoa elimu kuhusu madhara ya mimba na ndoa za utotoni. Aliwataka wajitume kwenye masomo yao darasani ili wawe na maisha mazuri.
Askari polisi kutoka dawati la jinsia na watoto wilaya ya Shinyanga Secilia Kizza akiwataka wanafunzi pale wanapofanyiwa ukatili wasiogope wala kuwaficha watuhumiwa ili washughulikiwe kisheria na kufungwa jela na hatimaye kukomesha vitendo hivyo vya kubebesha mimba wanafunzi na kukatisha ndoto zao. 
Meneja mradi wa kuzuia mimba na ndoa za utotoni kutoka Shirika la AGAPE Mustapha Isabuda akiwataka wanafunzi wa shule ya sekondari Mwamalili Manispaa ya Shinyanga kutafakari kwanini wapo shuleni hapo na wamefuata nini jambo ambalo litawafanya wajikite kwenye masomo tu na siyo mengine. 
Wanafunzi wa shule ya sekondari Mwamalili Manispaa ya Shinyanga,wakisikiliza nasaha kutoka kwa viongozi wa shirika la AGAPE namna ya kujinasua kukatishwa ndoto zao kwa kupaza sauti 
Wanafunzi wa shule ya sekondari Mwamalili Manispaa ya Shinyanga wakinyoosha mikono kuapa kuwa wote watafanya vizuri kwenye mitihani yao ya kuhitimu masomo kuwa hakuna atakayepata alama sifuri wala wanafunzi wa kike kukatishwa masomo kwa kuolewa ama kupewa ujauzito. 
Secilia Kizza kutoka dawati la jinsia na watoto jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga akiwasihi wanafunzi wa shule ya sekondari Mwamalili Manispaa ya Shinyanga kupaza sauti pale mtu ama ndugu yake akionyesha dalili za kufanya mchezo mchafu hata kwa wanafunzi wa kiume kulawitiwa watoe taarifa mapema ili ashughulikiwe. 

***** 
Shirika la Agape AIDS Control Programme la Mjini Shinyanga, linalotekeleza mradi wake waMradi wa Kuzuia mimba na ndoa za utotoni katika halmashauri ya manispaa ya Shinyanga na Shinyanga vijijini leo limetembelea shule ya msingi Ujamaa na shule ya sekondari Mwamalili zilizopo katika manispaa ya Shinyanga na kutoa elimu kwa wanafunzi namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi yao ambavyo vimekuwa vikikatisha ndoto zao.

Akizungumza katika shule ya msingi Ujamaa iliyopo katika kijiji cha Seseko kata ya Mwamalili pamoja na shule ya sekondari ya Mwamalili Meneja wa mradi huo Mustapha Isabuda aliwataka wananfunzi hao pale wanapoona dalili za kutaka kufanyiwa ukatili ama kutendewa kabisa, wasikae kimya bali watoe taarifa kwa wazazi wao, walimu ama viongozi wa serikali ili watu hao wapate kushughulikiwa.

Alisema hata kama mzazi wake anataka kumfanyia ukatili ama kuanza kumfanyia ukatili ikiwemo na kumkataza kwenda shule kwa ajili ya kuchunga mifugo au kwenda shambani kulima, wawe wajasiri kupinga suala hilo na kutoa taarifa kwa walimu, ili mzazi achukuliwe hatua za kisheria.

“Kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wazazi katika kata hii ya Mwamalili kukatisha masomo watoto wao kwa ajili ya kwenda kulima mashambani ama kuchunga mifugo jambo ambalo linapaswa kukemewa ikiwa hiyo ni njia mojawapo ya kuwafanya wanafunzi kufanya vibaya darasani na hatimaye kuolewa ndoa za utotoni,”alisema.

Aidha aliwataka wazazi na walezi kuithamini elimu kwani mpaka rais John Magufuli amefuta michango ili watoto wapate elimu bure, na kutoa wito kwao wawaache wanafunzi hao wasome na watimize ndoto zao ambapo hapo baadaye watakuja kuwasaidia na kuishi maisha mazuri.

Naye Mkurugenzi wa Shirika hilo la AGAPE John Myola alisema licha ya wanafunzi kutoa taarifa hizo pale mtu anapotaka kumbaka, anapaswa apige kelele ili kuepuka vitendo hivyo.

Pia aliwataka wanafunzi wa kiume kuwalinda dada zao kwa kutoa taarifa shuleni ama kwa wazazi wao pale wanapoona wenzao wakirubuniwa na mafataki wasikae kimya jambo ambalo nalo litasaidia kudhibiti mimba shuleni.

Kwa upande wake askari polisi kutoka dawati la jinsia na watoto Secilia Kizza aliwataka wanafunzi hao pindi wanapokuwa shuleni wajikite kwenye masomo na kuacha kujiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi katika umri mdogo pamoja na kuacha kwenda kwenye minada siku za mwisho wa wiki bali watumie muda huo kujisomea.

Nao wanafunzi hao waliiomba serikali kuwashughulikia wazazi ambao wamekuwa chanzo cha wanafunzi kukatishwa masomo, kwa kubebeshwa ujauzito kutokana na kuwakataza kwenda shuleni na kuamuriwa kwenda kuchunga mifugo ama kulima mashambani na hatimaye kukutana na vishawishi matokeo yake wanabakwa na kupewa mimba.

Baadhi ya wazazi katika kata hiyo ya Mwamalili Elizabeth Laurent na Peter Titus, kwa nyakati tofauti walikiri kuwepo na tabia hiyo kwa wenzao ambao wamekuwa kikwazo kwenye kampeni hizo za kutokomeza mimba na ndoa za utotoni ambapo wamekuwa wakiwazuia watoto wao kwenda shuleni na kuwaamuru kwenda mashambani ama kuchunga mifugo.

Walisema kutokana na kukithiri kwa vitendo hivyo tayari wameshaitwa kwenye vikao vya wazazi mashuleni ni kuonywa kuacha kufanya tabia hiyo bali wawaache wanafunzi wapate elimu na kuahidi kufanya hivyo, huku wakilaani kwa wale wazazi ambao wataendelea na vitendo hivyo.

Na Marco Maduhu - Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527