MAGEREZA WATAJA SABABU ZA KUMZUI PROFESA JAY KUMUONA SUGU GEREZANI

Mbunge wa Mikumi mkoani Morogoro, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ jana alizuiwa kumuona mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi pamoja na katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga baada ya kuzuiwa na maofisa wa magereza.


Profesa Jay aliyeambatana na mke wake, Grace Haule walifika jana jijini Mbeya na kwenda gerezani kuwaona Sugu na Masonga ambao wapo mahabusu wakikabiliwa na kesi ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.


Mkuu wa magereza Mkoa wa Mbeya, Kamshina Msaidizi Mwandamizi (SACP), Paul Kijida alisema walimzuia Profesa Jay kwa sababu haikuwa siku ya kuwaona mahabusu.


‘Kweli amekuja hadi ofisini kwangu, lakini taratibu hazipo hivyo. Siku za kawaida kama hizi tunamruhusu mtu anayempelekea chakula au ataruhusiwa pale mfungwa au mahabusu anaumwa au mwanasheria wake anaruhusiwa kama tu kuna kitu muhimu’’ alisema Kijida na kuongeza kwamba, 


‘’Lakini tukisema kila mtu kwa muda na siku anayotaka iwe siku ya kuwaona wafungwa au mahabusu hatutafanya kazi sasa. Siku za kuwaona wafungwa na mahabusu kwa watu wa kawaida ni Jumamosi na Jumapili tu,” alisema mkuu huyo wa magereza.


‘’Nimejaribu kuonana na RPO (mkuu wa magereza mkoa) lakini naye ameonekana kusita kunipa kibali cha mimi kuonana nao. 


"Na inaonyesha kuna kitu nyuma kimejificha. Lakini nimefunga safari kuja kuonana nao hivyo siwezi kuondoka bila kuonana hivyo kesho(leo) nitakuwepo mahakamani, nitazungumza nao,” alisema Profesa Jay jana.


Alisema anachotambua ni kuwa mbunge hazuiliwi kuwaona mahabusu gerezani, lakini jambo hilo limemshangaza.


Akizungumza na mama yake Sugu aitwaye Desderia, alimtaka kuwa na ustahimilivu katika kipindi hiki ambacho mwanaye yupo kwenye misukosuko.


Profesa Jay alisema, “mama usihofu, yule hajabaka wala hajaiba bali kilichomuweka ndani ni kutetea masilahi ya wananchi. Na ndio maana hata sisi tumeacha kazi zote huko kuja kuhakikisha tunashughulikia jambo hilo na naamini haki itatendeka tu. 


"Na hapa usione tupo wachache kuja hapa nyumbani, lakini Sugu ana kundi kubwa sana la watu na tumegawana majukumu ya kufanya kuhusu hili tatizo.”

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527