DC NDAGALA AZINDUA SHULE YA SEKONDARI BEREA ..AZITAKA SHULE BINAFSI KUJIKITA KATIKA MASOMO YA SAYANSI

Mkuu wa wilaya ya Kakonko mkoani Kigoma Kanali Hosea Ndagala amewataka wamiliki wa shule binafsi zinazoanzishwa wilayani humo kuhakikisha wanatoa elimu iliyo bora na kujikita katika masomo ya sayansi kwa kuwa hivi sasa nchi ya Tanzania inaingia katika uchumi wa viwanda na kuwasaidia vijana hao wapate ajira kwa urahisi.

Ndagala aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa shule ya sekondari Berea iliyoko wilayani humo ambapo aliwataka wamiliki kutafuta walimu wenye uwezo wa kufundisha masomo ya sayansi ili kupata wataalamu wa viwanda vitakavyoanzishwa kwakua mpango wa serikali ni kuifikisha nchi katika uchumi wa viwanda na ni lazima wazingatie utoaji wa elimu iliyo bora.

Aidha aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii na wasiridhike na kumaliza elimu ya kidato cha nne pekee, kwani huo ni msingi tu unaofungua maisha yao na kuwataka kusoma kwa bidii ili kufika mbali zaidi.


Aidha aliwaomba wananchi wa wilaya hiyo kuwa wazalendo kwa kuwaunga mkono wale wote wanaoanzisha shule kwa kuwapeleka watoto wakapate elimu na kuacha kuwakatisha tamaa wale watu wanaotaka kuwekeza kwa maneno ya kejeli kwani hali hiyo inasababisha wilaya hiyo kushindwa kuinuka kiuchumi.

"Niwatie moyo wote mnaotaka kuwekeza katika wilaya hii serikali ipo kwa ajili ya kuwatia moyo na serikali inahitaji wawekezaji najua mnakatishwa tamaa lakini nikupongeze mmiliki wa shule hii ni changamoto nyingi umepitia lakini hukukata tamaa umekuwa mzalendo kuja kuwekeza nyumbani, changamoto hizo zifanye kuwa fursa ili tuweze kuhakikisha wilaya yetu inainuka katika elimu na uchumi kwa ujumla", alisema Ndagala.

Kwa upande wake mkurugenzi wa shule ya Berea Baraka Mathias alisema anaishukuru sana serikali kwa ushirikiano aliopata ikiwa ni pamoja na kupatiwa usajili wa shule hiyo na kuwaomba wananchi kuacha tabia ya kuwavunja moyo wale wote wenye nia ya kuinua wilaya ya Kakonko kwa kuleta maendeleo.

Pia aliwataka vijana kusimamia malengo yao na ndoto walizonazo kuziishi ili kufanikisha mipango yao na kuwaomba wawekezaji wengine kuwekeza katika wilaya hiyo ambayo imesahaulika ili kuweza kufungua fursa na kusaidia kuinua uchumi wa Wana Kakonko.

Alisema shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 103 na ni moja kati ya shule zinazofanya vizuri kwenye mitihani wilayani humo na kwamba pamoja na changamoto zote hakukata tamaa, alihakikisha anasimamia wazo lake la kuanzisha shule katika ili wanafunzi wapate elimu kwa ukaribu zaidi.

Na Rhoda Ezekiel- Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akizungumza wakati wa kufungua shule ya Sekondari Berea -Picha na Rhoda Ezekiel- Malunde1 blog
Mkuu wa wilaya ya Kakonko Kanali Hosea Ndagala akikata utepe kufungua shule ya Sekondari Berea


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527