CHOO CHAWAGONGANISHA MKUU WA WILAYA, DED...SHULE YAFUNGWA


Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili
****
SHULE ya Msingi Bunda A na B iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Bunda mkoani Mara, imefungwa kwa kipindi cha wiki mbili kutokana na choo cha shule hiyo kujaa kutitia na kubomoka.

Hatua hiyo imeelezwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Lydia Bupilipili imesababishwa na uzembe wa watumishi wa halmashauri hiyo. Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake, Bupilipili alisema kuwa anasikitishwa na kitendo cha shule hiyo kufungwa na kusema kuwa lazima wote waliozembea watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Shule hiyo imefungwa juzi na uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, kwa kile kinachoelezwa kuwa hali hiyo ingehatarisha afya na maisha ya wanafunzi waliokuwa wanakwenda kujisaidia katika choo hicho.

Ilielezwa kuwa kutokana na hali hiyo ya ukosefu wa choo, wanafunzi walikuwa wanalazimika kujisaidia sehemu ambayo si rasmi na kwenye vichaka vya mlima wa jirani kwenye eneo lililoko jirani na makao makuu ya Wilaya ya Bunda. Kufuatia shule hiyo kufungwa, Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa hali hiyo inatokana na uzembe wa baadhi ya watumishi halmashauri hiyo, kwa kutolishughulikia mapema tatizo hilo, hasa kipindi ambacho shule zilikuwa zimefungwa.

“Huo ni uzembe kwani pale shuleni kulikuwa hakuna walimu? Au Mratibu Elimu Kata? Au Ofisa Elimu na hata Mkurugenzi mpaka shule inajaa bila kuchukua hatua mapema? “Na ni kwa nini wasingeijenga wakati ambao shule zilikuwa zimefungwa, sasa wanafunzi wanafungua ndipo wanaifunga, eti waanze ujenzi, hili haliniingii akilini kabisa,” alisema Bupilipili.
Chanzo- Habarileo

Alisema kuwa tayari amekwishawaandikia barua watumishi wote waliozembea, akiwemo Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Janeth Mayanja ili waweze kujieleza na kwamba wahusika watawajibishwa, kwani wamesababisha wanafunzi hao kukosa haki yao ya kupata elimu.

Aliongeza kuwa; “kwani halmashauri hiyo haina uwezo wa kujenga choo hicho, wakati wanakusanya mapato mengi tu, lazima wawajibike na tayari barua za kujieleza nimekwishawaandikia wote. “Kwanza haya mamlaka ya kuifunga shule hiyo waliyatoa wapi, maana hawana mamlaka ya kufunga shule,” alisema Bupilipili.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527