Picha : WAKURUGENZI WA HALMASHAURI ZA WILAYA MKOA WA MARA WAIMWAGIA SIFA AGPAHI




Mwenyekiti wa Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya mkoa wa Mara,Charles Kitamuru Chacha.
**
Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya mkoa wa Mara wamelipongeza Shirika la Ariel Glaser Pediatric AIDS Healthcare Initiative (AGPAHI) kwa kutekeleza kikamilifu mradi wa “Boresha” unaotoa huduma za kinga, tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU na Ukimwi mkoani humo.

Pongezi hizo zimetolewa Januari 23,2018 na Mwenyekiti wa Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya mkoa wa Mara, Charles Kitamuru Chacha ambaye ni Mkurugenzi wa halmashauri ya Rorya wakati akifunga mafunzo kuhusu taratibu na kanuni za matumizi ya fedha za wafadhili ‘Watu wa Marekani kupitia Centres for Disease Control (CDC)’.

Mafunzo hayo ya siku mbili kuhusu taratibu na kanuni za matumizi ya fedha za wafadhili yaliyoanza Januari 22,2018 hadi Januari 23,2018 yalifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mwembeni na kuhudhuriwa na wakurugenzi na viongozi wa timu za afya za mikoa na wilaya.

Mwenyekiti huyo wa wakurugenzi alisema shirika la AGPAHI limekuwa msaada mkubwa katika sekta ya afya kwenye halmashauri za wilaya mkoani humo hususani katika miradi yake ya Ukimwi na kusisitiza kuwa halmashauri zote zitaendelea kuunga mkono shughuli zinazofanywa na AGPAHI.

“Kwa niaba ya wakurugenzi wenzangu nikiwa kama mwenyekiti wa wakurugenzi wa halmashauri za wilaya mkoani hapa, natoa shukrani za pekee kwa wadau wetu AGPAHI na Watu wa Marekani kupitia CDC kwa shughuli mnazofanya kufanikisha huduma za kinga, tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU na Ukimwi”, alieleza Chacha.

“Shirika hili limekuwa la mfano katika masuala ya Ukimwi na kila mtu mkoani hapa amekuwa na mtazamo chanya na AGPAHI, ndiyo maana tumekuwa tukiwashirikisha hata kwenye vikao vyetu vya mkoa ikiwemo Baraza la Ushauri la mkoa (RCC) na kuwapa nafasi ya kueleza mambo wanayofanya”,aliongeza Chacha.

Aidha alitumia fursa hiyo kuziomba halmashauri za wilaya kutumia vizuri fedha za wafadhili shilingi bilioni 7.2 zilizotolewa na AGPAHI mwaka huu kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Boresha mkoani Mara huku akisisitiza uwasilishwaji wa taarifa za mradi kwa wakati.

Naye Meneja wa Shirika la AGPAHI Kanda ya Ziwa, Dk. Nkingwa Mabelele alizishukuru halmashauri za wilaya na serikali ya mkoa wa Mara kwa ushirikiano wanaotoa katika kuhakikisha kuwa malengo ya shirika hilo kutekeleza miradi ya Ukimwi yanafanikiwa.

Kwa upande wake, Afisa Ruzuku Mwandamizi wa shirika la AGPAHI, Leticia Gilba alisema mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo wakurugenzi wa halmashauri na timu za afya za mkoa na wilaya kuhusu namna ya kutumia fedha za mfadhili sawa sawa na matakwa na makubaliano kati ya AGPAHI na serikali ya Marekani.

Alisema miongoni mwa mada zilizotolewa wakati wa mafunzo hayo kuwa ni vigezo na masharti ya mkataba wa utekelezaji wa mradi wa Boresha, taratibu za matumizi ya fedha za wafadhili, uandaaji wa ripoti na viambatanisho sahihi vya malipo pamoja na utunzaji wa rasilimali. 

Washiriki wa mafunzo hayo walikuwa wakurugenzi wa halmashauri za wilaya Mji wa Bunda na Tarime Mji, Manispaa ya Musoma, Bunda Vijijini, Butiama, Musoma Vijijini, Rorya,Tarime Vijijini na Serengeti na timu za afya za mkoa na wilaya.

ANGALIA PICHA WAKATI WA KUFUNGA MAFUNZO 
Mwenyekiti wa Wakurugenzi wa halmashauri za wilaya 9 za mkoa wa Mara, Charles Kitamuru Chacha akizungumza wakati wa kufunga mafunzo kuhusu taratibu na kanuni za matumizi ya fedha za wafadhili "Watu wa Marekani kupitia CDC" katika ukumbi wa Mwembeni uliopo katika manispaa ya Musoma. Kushoto ni Mratibu wa Ukimwi mkoa wa Mara, Dk.Oning'o Felix.
Chacha akiwasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia mambo waliyojifunza ili kuboresha utendaji kazi kwenye maeneo yao.
Mratibu wa Ukimwi mkoa wa Mara, Dk. Oning'o Felix akilishukuru shirika la AGPAHI kwa kuwapatia mafunzo hayo ambayo yatawasaidia kuboresha huduma katika vituo vya afya.
Meneja wa Shirika la AGPAHI Kanda ya Ziwa, Dk. Nkingwa Mabelele akizishukuru halmashauri za wilaya na uongozi wa mkoa wa Mara kwa kuendelea kushirikiana na AGPAHI kutekeleza miradi ya Ukimwi mkoani humo.
Afisa Ruzuku Mwandamizi wa shirika la AGPAHI, Leticia Gilba akiwapongeza washiriki wa mafunzo hayo kwa kuwa wasikivu katika mada zote zilizotolewa kwa muda wa siku mbili.
Washiriki wa mafunzo hayo wakiwa ukumbini.
Mratibu wa AGPAHI mkoa wa Mara, Alio Hussein akitoa neno la shukrani wakati wa kufunga mafunzo hayo.

PICHA ZA MATUKIO KABLA YA KUFUNGA MAFUNZO
Afisa Ruzuku wa AGPAHI mkoa wa Mara, Sabure Mtatiro akitoa mada kuhusu utunzaji wa rasilimali.
Washiriki wa mafunzo wakifuatilia mada ukumbini.
Afisa Ruzuku wa AGPAHI mkoa wa Mara, Godfrey Sindabaha akitoa mada kuhusu uandaaji wa ripoti.
Washiriki wakifuatilia mada ukumbini.
Leticia Gilba akitoa mada kuhusu viambatanisho sahihi vya malipo.
Washiriki wa mafunzo wakiwa ukumbini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527