WABUNGE TANZANIA WATAKIWA KUWASILISHA TAARIFA ZAO ZA MIAMALA YA BENKI

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imewaandikia barua baadhi ya wabunge, ikiwataka kuwasilisha taarifa za miamala ya benki za kuanzia Januari hadi Desemba 2017.


Sekretarieti hiyo imetaka taarifa hizo ziwe zimeifikia ndani ya siku 30 kuanzia Januari 15, 2018.


Barua hiyo inawataka wabunge hao kutekeleza agizo hilo ili kuthibitisha taarifa zilizomo kwenye tamko lake alilowasilisha.


Ofisa mmoja wa taasisi hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe, alithibitisha kuwepo kwa barua hizo, akisema si wote walioandikiwa barua za kutakiwa kutoa taarifa hizo.


Hata hivyo, alisema wabunge walioandikiwa ni wale ambao fomu zao zinaonyesha haja ya uhakiki zaidi wa taarifa zao.


Rais wa John Pombe Magufuli ndiye alikuwa wa kwanza kuwasilisha fomu yake ya tamko kuhusu rasilimali na madeni katika ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyopo Mtaa wa Ohio, Wilaya ya Ilala Jijini Dar es Salaam Desemba 28, 2017.


Baada ya kuwasilisha fomu hiyo, Rais aliipongeza sekretarieti hiyo kwa kazi inazofanya na kumtaka Kamishna wa Maadili Jaji Mstaafu, Harold Nsekela kutopokea fomu ya kiongozi yeyote ambaye angeshindwa kuwasilisha tamko la kabla ya Desemba31, 2017.


Kauli hiyo ya Rais iliwaamsha viongozi mbalimbali wakiwemo wabunge na viongozi wengine wa Serikali kufurika kwenye ofisi hiyo kuwasilisha matamko yao ya mali walizonazo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527