TRAFIKI ANASWA AKIOMBA RUSHWA MWANAFUNZI


POLISI wa kikosi cha usalama barabarani nchini Kenya, amenaswa akiomba rushwa kwa mwanafunzi Mganda, aliyekuwa akiendesha gari kwenye eneo la Narok.


Jeshi la Polisi Kenya limesema polisi huyo ametambulika na mchakato wa kumfukuza kazi unaendelea. 

Picha za video zinamwonesha mtumishi huyo wa umma akiwa pembeni ya gari la mwanafunzi huyo na pia mazungumzo yao yanasikika akishinikiza apewe fedha ili amwachie dereva huyo wa kiume.

Kwa kuzingatia mazungumzo hayo, mwanafunzi huyo alisimamishwa kwa kosa la kuendesha gari kwa mwendo kasi kupita kiasi. Wakati wa mazungumzo hayo, polisi alimweleza dereva kuwa “Nimeenda Kampala mara mbili…kuna ofisa wa jeshi, trafiki, na mkusanya mapato, si ndiyo? Wanasimama watu watatu, fedha papo hapo”.

Dereva huyo alimjibu “Ofisa, hii ni mara yangu ya kwanza kuja Kenya”. Polisi akamjibu kwa kumkatiza “Lete, lete, lete fedha hapa nikusaidie unavyotaka”. Baada ya kutamka hayo polisi huyo akacheka.

Dereva huyo anaonekana akitoa fedha na akamuuliza polisi “kiasi gani?. Polisi akamjibu “Sio fedha ndogo ndogo, hapa hatuchukui hizo fedha ndogo ndogo” Dereva huyo alimjibu kwamba hakuwa na fedha nyingi, kwa kuwa alikuwa amebadilisha fedha kidogo.

“Tunachukua maelfu, kama una elfu mbili nitachukua,” alisema polisi huyo. “Unaweza ukaniachia angalau kiasi kidogo” aliuliza dereva huyo. Polisi huyo alikataa. “Hapana, elfu moja, lete elfu moja (huku akitazama nyuma yake), fanya haraka, haraka… haraka, haraka nakwenda (anapokea fedha), hiki ni kiasi gani?” aliuliza polisi huyo.

“Sijui, nimekupa nilichokuwa nacho,” alimjibu dereva huyo. “Ndogo sana, lakini wewe ni mgeni, nenda, wewe ni mgeni, sitaki kufanya maisha yawe magumu kwako, asante,” alisema Polisi huyo.

Mkuu wa Polisi Kenya (IGP), Joseph Boinnet alikaririwa akisema kuwa, polisi huyo atafukuzwa kazi kwa kuzingatia sera ya jeshi hilo kutovumilia rushwa.
Chanzo- Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527