DIAMOND KUJENGA KIWANDA CHA KARANGA UGANDA


MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya, Nassib Abdul ‘Diamond Platinumz’ wa Tanzania, anakusudia kuwekeza nchini Rwanda kwa kujenga kiwanda cha karanga nchini humo.

Kijana huyo pia anatafuta nyumba ya kuishi jiji Kigali kwa kuwa jiji hilo ni salama, safi na anamkubali sana Rais Paul Kagame. Kwa mujibu wa msanii huyo, atakapofungua kiwanda kitatoa fursa za ajira na kwamba lengo la biashara yake ni zaidi ya soko.

”…nitafurahi zaidi kama watu watafurahia bidhaa zangu, lakini zaidi wakipata ajira na kubadili hali ya maisha yao,” alisema wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Kigali. Msanii huyo alikwenda Kigali Ijumaa asubuhi kwa safari ya kibiashara na kijamii.

Alisema, wasanii wanapaswa kufanya muziki si tu kuburudisha, lakini pia uwe chanzo cha biashara inayoweza kuwanufaisha watu wengi. “Kuna uwezekano kwa vijana wengi kunufaishwa na biashara zetu (wanamuziki), iwe kwenye kazi za mauzo yetu au hata kutengeneza ajira kwa ajili yao mara kiwanda kikianza kazi,” alisema Diamond.

Alisema, alikwenda jijini humo kusalimia mashabiki wake mtaani na kuwaonesha kuwa sasa amekua. “Nipo nilivyo kwa sababu ya muziki wangu. Nimefanikiwa sana, naushukuru muziki.

Kwa sasa nina Diamond Karanga, manukato ya Chibu na Wasafi Records. Nataka pia kufungua Wasafi FM na Wasafi TV nchini Tanzania,” alisema Diamond. Alisema amepata mafanikio kwa sababu ya kufanya kazi kwa bidii, watu anaoshirikiana nao, ubunifu na heshima.

Kupitia vyote hivi nipo tayari pia kusaidia vijana kukuza vipaji vyao viwe vya kiwango cha juu kuendeleza muziki wa Afrika,” alisema. Jumamosi Diamond alikwenda kwenye maeneo mbalimbali ya katikati ya jiji la Kigali kutafuta nyumba ya kununua.

Alikwenda kuona nyumba kwenye maeneo ya Nyarugenge na Kimihurura.“Mashabiki wangu Kigali kila mara wananiona jukwaani, nimevaa miwani lakini sasa nataka nitembee kwenye mitaa ya Kigali, niwasalimie kuwaonesha kwamba kwa kweli nimekua,” alisema wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Nyota huyo wa muziki aliwasili Kigali asubuhi kwa mwaliko wa Taasisi ya Jordan, inayojitolea kusaidia watoto wenye matatizo ya kuona kwenye eneo la Gatsata wilayani Gasabo. Taasisi hiyo ilianzishwa na Vanessa Bahati kusaidia wenye matatizo ya kuona.
Chanzo- Habarileo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527