SERIKALI KUKUSANYA TRILIONI 32.4 BAJETI YA MWAKA 2018/2019

 Serikali inatarajia kukusanya na kutumia Sh 32.4 trilioni katika bajeti ya mwaka 2018/19.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango amesema leo wakati akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2018/19 na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2018/19 bungeni mjini hapa.

Mpango amesema mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa zaidi ya Sh 22 trilioni sawa na asilimia 68 ya mahitaji yote.

"Washirika wa maendeleo wanatarajia kuchangia Sh 3.7 trilioni katika bajeti," amesema Dk Mpango.

Amesema Sh 20.2 trilioni ni fedha za matumizi ya kawaida wakati maendeleo ni Sh 12.2 trilioni.

Amesema Sh  7.6 trilioni zitatumika kwa ajili ya kulipa mishahara ya watumishi wa Serikali na taasisi za umma katika mwaka huo.

Amesema vipaumbele vya serikali ni vinne vya mpango wa maendeleo wa Taifa wa mwaka wa fedha 2018/ 19.

Amesema Sh 9.7 trilioni kutumika kulipa deni la Taifa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/19.

Amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni kukuza uchumi na ujenzi wa msingi wa uchumi wa viwanda, kugungamanisha uchumi na maendeleo ya watu, ujenzi wa mazingira wezeshi kwa uendeshaji biashara na uwekezaji na kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa mpango.

Dk Mpango amesema deni la Taifa limeongezeka kufikia dola 26,115.2 Juni mwaka huu ikiwa ni ongezeko la asilimia 17 ikilinganishwa na dola 22,320.76 za kimarekani Juni mwaka jana.

Dk Mpango amesema msukumo mkubwa utaweka katika mikakati ya kuongeza mapato, kupunguza gharama na matumizi ya uendeshaji wa Serikali na kudhibiti ulimbikizaji wa madeni- Waziri wa Fedha na Mipango Dk Philip Mpango.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527