GAVANA WA KENYA AFARIKI KATIKA AJALI YA GARI


Gari ikiwa imepata ajali


Gavana wa kaunti ya Nyeri nchini Kenya Wahome Gakuru amefariki mapema siku ya Jumanne kufuatia ajali mbaya ya gari barabarani katika eneo la Kabati katika barabara kuu ya Thika-Sagana katika kaunti ya Murang'a.

Alikimbizwa katika Hospitali ya Thika Level 5 kwa matibabu ya dharura lakini akaaga dunia.
Kaunti kamishna wa Murang'a John Elungata alithibitisha kifo hicho.

Bwana Elungata alisema kuwa kabati ni eneo hatari na madereva hukosa mwelekeo kila kunaponyesha.

Maafisa wa polisi wanasema kuwa gari la gavana huyo lilikuwa na abiria wanne wakati wa ajali hiyo ,akiwemo msaidizi wake wa kibinafsi, mlinzi wake na Dereva.

Mkono na mguu wa msaidizi wake wa kibinafsi ilivunjika huku miguu ya mlinzi wake ikijeruhiwa vibaya huku Dereva akidaiwa kuwa katika hali nzuri.Mapema siku ya Jumatatu alipiga picha na wanafunzi wa shule ya upili ya Alliance Boys wanaokalia mtihani wa kidato cha nne

Polisi wanasema kuwa ajali hiyo ilitokea baada ya gurudumo moja la gari hilo kupasuka wakati mvua kali ilipokuwa ikinyesha.

Mwili wa Gavana huyo umesafirishwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee mjini Nairobi.

Inadaiwa kuwa Gavana huyo alikuwa akielekea kuhudhuria kipindi kimoja cha radio na runinga wakati gari lake lilipokumbwa na ajali hiyo.

Daktari Gakuru ni Gavana wa pili wa Nyeri kufariki afisini baada ya Gavana Nderitu Gachagua kufariki mwezi Februari mwaka huu.

 Chanzo-BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527