KESI YA VIGOGO WA SIMBA YAAHIRISHWA HADI OKTOBA 11

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeahirisha kesi ya utakatishaji fedha na kugushi inayowakabili Rais wa Simba, Evans Aveva na Makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ hadi October 11, 2017 kwa sababu upelelezi haujakamilika.


Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Leornad Swai amemueleza Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa kuwa shauri hilo limeitishwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika, hivyo anaomba ipangiwe tarehe nyingine ambapo baada ya kueleza hayo Hakimu Mwambapa aliahirisha kesi hiyo hadi October 11, 2017.


Evans Aveva na Makamu wake, Geofrey wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha Dola za kimarekani 300,000.


Katika shtaka la kwanza, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa walikula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya March 15, 2016 wakionesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa Dola za kimarekani 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli.


Katika shtaka la pili alidai kuwa March 15, 2016 katika benki ya CRDB tawi la Azikiwe Ilala, Aveva akijua alitoa nyaraka ya uongo ambayo ni fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya March 15, 2016 wakati akijua ni kosa.


Katika la tatu la kutakatisha fedha, Aveva na Nyange wanadaiwa kuwa kati ya March 15 na June 29, 2016 Dar es Salaam kwa pamoja walikula njama ya kutakatisha fedha kwa kupata Dola za kimarekani 300,000 wakati wakijua ni zao la uhalifu.


Kwa upande wa shtaka la nne la kutakatisha fedha, Aveva anadaiwa kuwa kati ya March 15, 2016 katika benki ya Barclays Mikocheni alijipatia Dola za kimarekani 300,000 wakati akijua zimetokana na kughushi.


Katika shtaka la tano la kutakatisha fedha, mshtakiwa Nyange anadaiwa kuwa March 15, 2016 katika benki ya Barclays tawi la Mikocheni alimsaidia Aveva kujipatia Dola za kimarekani 300,000 wakati akijua fedha hizo zimetokana na kughushi.


Washtakiwa wapo rumande kwa sababu shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments