Jukwaa la Katiba (Jukata) limemuomba Rais John Magufuli apokee maandamano ya amani kushinikiza kufufua mchakato wa Katiba mpya.
Jukata
limefikia maamuzi ya kufanya maandamano hayo ya amani nchi nzima
kutokana na makubaliano ya mkutano mkuu wa dharura wa jukwaa hilo
uliofanyika Septemba 29 mjini Dodoma ambao pamoja na mambo mengine
ulikubaliana kuyafanyia kazi maoni ya wananchi ambayo yamekuwa
yakisisitiza kuwapo kwa mchakato wa Katiba mpya.
Hata
hivyo hivi karibuni Kurugenzi wa Mawasiliano ya Rais ilizitaarifu
taasisi za umma na zisizo za umma zinazomualika Rais Magufuli
kutotangaza ushiriki wake hadi zipate uthibitisho kutoka Ofisi ya Rais.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Jumamosi, Mwenyekiti
wa Jukata, Hebron Mwakagenda alisema maandamano hayo ya amani
yatafanyika nchi nzima Oktoba 30.
Alisema tayari wamemuandikia barua Rais Magufuli ya kutaka ayapokee maandamano hayo ya amani wakiwa na ujumbe mahususi kwake.
Alifafanua
sababu ya kumuomba Rais apokee maandamano hayo ni kumkumbusha kuwa
mambo yote mazuri anayoyafanya ikiwamo kupiga vita rushwa, kusimamia
matumizi mabaya ya mali za umma, yanaweza yasilete tija na maendeleo
endelevu na ya muda mrefu kwa sababu mengi yanakosa msingi wa kikatiba.
"Akumbuke
kuwa yeye siyo Rais wa kudumu, kama asipojenga mifumo imara anayefuata
anaweza kuyafuta kirahisi masuala yote mazuri na kuirudisha nchi kwenye
hali mbaya kama ambavyo amekuwa akidai.”
"Katiba
ndiyo suluhisho la kulinda mazuri yote anayoyafanya na kujenga mifumo
thabiti isiyoruhusu nchi kuchezewa na watu wachache kwa manufaa yao,"
alisema.
Amesema
kuna umuhimu wa kuyaweka masuala yote yanayofanyika sasa katika Katiba
kutokana na ukweli kwamba Katiba ndiyo sheria mama na dira ya nchi.
"Imethibitika
bila shaka, nchi zenye Katiba bora ustawi wa Taifa huwa wa hali ya juu
kuliko nchi zilizokuwa na migogoro kutokana na kukosa Katiba zenye
misingi ya uongozi," amesema Mwakagenda.
Mwakagenda
alifafanua kuwa maandamano hayo katika ngazi ya kitaifa yatafanyika
jijini Dar es Salaam na yataanzia kwenye ofisi za Jukata na kumalizikia
viwanja vya Mnazi Mmoja.
Alisema
kwa upande wa mikoani nje ya Dar es Salaam kila wilaya ya Tanzania
wameshapeleka taarifa kwa wakuu wa Polisi wa Wilaya kuwafahamisha kuhusu
njia yatakapopita maandamano hayo ya amani.
"Lengo
la taarifa hiyo mikoani ni kuwaomba wakuu wa wilaya ambao ni
wawakilishi wa Rais kwenye wilaya husika kuyapokea," alisema Mwakagenda.
Mwakagenda alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kushiriki kwenye maandamano hayo ya amani.
Alisema
maandamano ni njia mojawapo ya wananchi kuwasiliana na viongozi wao
ambao wamepewa dhamana ya kuongoza Taifa kwa mujibu wa Katiba na sheria
za nchi.
Alieleza
Jukata wana imani watapata ushirikiano wa kutosha kutoka Jeshi la
Polisi nchini ili maandamano hayo yafanyike katika hali ya amani na
utulivu.
Alisema
ana imani wananchi pia watapokea kwa mtizamo chanya kusudio la kufanya
maandamano hayo yenye lengo la kurudisha hamasa ya wananchi kushiriki
kwenye michakato ya kidemokrasia.
“Hamasa
imepungua, iwapo wananchi watapoteza hamasa hiyo kabisa, ipo hatari
huko mbele michakato mingine kama uchaguzi kukosa ushiriki kutokana na
wananchi wengi kutoona umuhimu wa kushiriki mambo muhimu ya nchi
yao,”alisema.
Alisema
Tanzania itakuwa nchi ya viwanda ikiwa kipaumbele kitakuwa Katiba mpya
yenye mifumo imara ili kusafiri katika njia sahihi wananchi waitakayo.
“Bila
Katiba mpya na bora ni sawa na kujenga nyumba nzuri juu ya mchanga
ambayo inaweza kuangushwa hata na upepo, ” alisema Mwakagenda.

Social Plugin