Updates: WATANO WAKAMATWA NA POLISI KWA KUMUOMBEA TUNDU LISSU

Jeshi la Polisi jijini Dar es salaam, linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kuratibu shughuli za maombezi maalum kwa ajili ya mbunge Tundu Lissu, katika viwanja vya TIP Sinza.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi mkoa wa Kinondoni Murilo Jumanne aliyekuwa eneo la tukio, amesema wameamua kuwakamata watu hao kwa kuwa wanatishia amani na utulivu wa nchi.

"Wale wenye nia mbaya ambao bila shaka wana ajenda binafsi ajenda ambazo kimsingi zina uelekeo wa kutishia masuala ya amani, mimi kama Kamnda wa Polisi mkoa wa Kinondoni, siwezi kukubali hali hiyo itokee kwenye eneo langu, watu wanaendelea na shughuli zao na wachache wakiwa wamevaa nguo za kawaida lakini wameficha tishirt ndani, wanafika sehemu wanaanza kuzitoa", amesema Kamanda Jumanne.

Kamanda Jumanne ameendelea kwa kuwataka wananchi kuacha kufanya mikusanyiko ya aina hiyo, na iwapo wanahitaji kufanya ibada waende kwenye sehemu za ibada.

Jana Jeshi la polisi Kanda maalum lilitoa taarifa ya kupiga marufuku kusanyiko lolote lisilo halali kumuombea Mbunge Tundu Lissu ambaye yuko Nairobi kwa matibabu, na kusema ni kuhatarisha hali ya amani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527