LAZARO NYALANDU AMTEMBELEA TUNDU LISSU KENYA

Mbunge wa Singida Kaskazini Mhe. Lazaro Samuel Nyalandu amemtembelea Mbunge wa Singida Mashariki Mhe. Tundu Lissu jijini Nairobi nchini Kenya kumjulia hali kufuatia mbunge huyo kupigwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 akiwa mjini Dodoma.

Lazaro Nyalandu amesema kuwa kwa niaba ya watu wa Singida na Watanzania wote ametoa salamu za pole kwa mke wa Tundu Lissu kwa kuwa bado hajapata nafasi ya kumuona kiongozi huyo na kusema anasubiri kama ataweza kupata nafasi ya kumuona usiku wa leo kama madaktari wataruhusu.

"Nimefika hospitali ya Nairobi mapema leo kumjulia hali Mh. Tundu Lissu madaktari wanaendelea kumfanyia matibabu, na bado hatujaruhusiwa kumuona. Kwa niaba ya wana Singida na Watanzania wote, nimetoa salaam za pole kwa mke wake, na bado nasubiri uwezekano wa kuweza kuonana naye usiku wa leo endapo madaktari wataruhusu" alisema Nyalandu

Aidha Mbunge huyo amewataka Watanzania kijumla kuendelea kumuombe Mbunge Tundu Lissu ili aweze kupona na kurejea nchini akiwa mzima wa afya njema

"Cha muhimu zaidi, sote tuendelee kumuombea Mungu amtendee wema, na kumponya katika majira haya ya kujaribiwa kwake. Katika yote ndani ya yote, ikawe heri kwake" alisema Nyalandu

Mbunge Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, 2017 akiwa Makao Makuu ya nchi jijini Dodoma na baadaye kusafirishwa kupelekwa jijini Nairobi Kenye kwa matibabu ambapo mpaka sasa yupo huko akiendelea kupata matibabu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527