Picha : BASI LA ALLYS LAPINDUKA, LAUA NA KUJERUHI WATU 25 SHINYANGA




Basi la Kampuni ya Allys Sports lenye namba za usajili T.979 CDH lililokuwa linatoka Ushirombo kwenda Bariadi mkoani Simiyu limepinduka katika eneo la Maganzo mkoani Shinyangana kusababisha kifo cha abiria mmoja Lukas Maganga (25) na kujeruhi wengine 25.


Ajali hiyo imetokea leo Septemba 25,2017 majira ya saa nne asubuhi katika eneo la Maganzo barabara ya Shinyanga kwenda Mwanza.

Inaelezwa kuwa basi lilikuwa katika mwendokasi, lilizidisha abiria na dereva alikuwa anaongea na simu na mara baada ya gurudumu la mbele la basi kupasuka alishindwa kulimudu na kupinduka.

Mashuhuda wa ajali hiyo wameeleza kuwa dereva wake Salumu Mseke alikuwa akiendesha basi hilo kwa mkono mmoja huku akiongea na simu ya mkononi.

Majeruhi walionusurika kwenye ajali hiyo Donald Supila, alisema basi hilo lilikuwa limezidisha abiria kama 20 na kufikia idadi yao kuwa  70, ambapo wastani ilitakiwa kubeba watu 50, na walipofika eneo la Kagongwa Kahama askari wa usalama barabarani aliwashusha lakini wakafaulishwa tena na kuendelea na safari kwenda Bariadi.

“Tulivyoona mwendo wa dereva siyo mzuri tulimzuia kutoendesha mwendo kasi na kuongea na simu lakini hakutujali,tukakwaruzana naye, na tulipofika eneo hilo la Maganzo ndipo tukapata ajali”,aliongeza Supila.

Naye Juliety Samweli alisema, wakati basi hilo likiendelea na safari ilifikia kipindi dereva akawa anaendeshea kwa mkono mmoja huku akiongea na simu akicheka na marafiki zake na kila akisimamishwa na askari wa usalama barabarani alikuwa akiongea nao na kisha kumwachia huku abiria wakiwa wamerundikana na hatimaye kupata ajali.

Majeruhi 25 katika ajali hiyo walikimbizwa katika hospitali ya Mwadui, Kolandoto na hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga  kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi na hali zao zinaendelea vizuri.

Kaimu kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga (RCO) Amedeus Tesha alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kubainisha kuwa wanamsaka dereva wa basi hilo ambaye alikimbia baada ya kutokea kwa ajili hiyo na wakimkamata watamfikisha mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.
Basi la Allys Sports likiwa kimepinduka
Tairi likiwa limepasuka
Uokoaji ukiendelea
Basi baada ya kuinuliwa

Picha zote na Ommy Fashion

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527