CCM MBEYA YAWAPA POLE WAATHIRIKA WA MOTO ULIOTEKETEZA SOKO LA SIDO


Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya,Wilson Nkhambaku.
***
Chama cha mapinduzi mkoa wa Mbeya kimetoa pole kwa wafanyabiashara waliopoteza mali zao kufuatia janga la moto ulioteketeza soko la SIDO Agosti 15,2017.


Akitoa taarifa ya chama hicho kwa waandishi wa habari,leo Katibu wa CCM mkoa wa Mbeya,Wilson Nkhambaku, alisema Chama Cha Mapinduzi kimeelezea masikitiko yake kutokana na kuungua kwa soko-tegemeo la SIDO.

 "Tukio hili si tu limewaumiza na kuwasononesha wafanyabiashara wa SIDO, bali limekiumiza Chama chetu Cha Mapinduzi, serikali, taasisi, mbalimbali na wananchi wote kwa ujumla" ,alisema  Nkhambaku.
Alisema athari za kuungua moto soko la SIDO  ni kubwa kiuchumi, kiusalama, kijamii na kisaikolojia.

"Wapo wafanyabiashara waliokuwa na mikopo kwenye mabenki na taasisi nyingine za kifedha ambao sasa watakuwa na wakati mgumu kurejesha mikopo yao, ni kwa msingi huo Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Mbeya kinaungana na taasisi zingine kuwapa pole sana wafanyabiara ambao mali zao zimeteketea kwa moto",alieleza.


Aidha, alisema Chama Cha Mapinduzi kupitia kwa wabunge wake mkoani Mbeya, na hasa mbunge wa viti maalum Dr. Mary Mwanjelwa, wote wametuma salamu nyingi za pole kwa wafanyabiashara na wajasiriamali ambao wamepoteza mali zao.
  
Nkhambaku alisema kufuatia tukio hilo Chama Cha Mapinduzi kimeshaiagiza serikali ya mkoa kuunda tume ya uchunguzi ili kuweza kubaini nini chanzo cha moto huo na pia hasara iliyotokana na janga hilo.
  
"Chama kimeielekeza serikali kuhakikisha kwamba tume hiyo inafanya kazi kwa umakini, uadilifu na ndani ya siku tano kuanzia tarehe 16-21/8/2017 iwe imeshakamilisha kazi hiyo na kutoa taarifa",alieleza Nkhambaku.

Alisema tayari  tume ya watu 9 imeshaundwa na iko kazini kufuatilia suala hilo.

Alisema Chama cha mapinduzi kimetoa wito kwa wafanyabiashara walioathirika na janga hilo na wananchi wote wa Mbeya kikiwasihi sana waendelee kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati serikali ikishughulikia jambo hilo.

Aidha alisema CCM alihahakikishia wananchi wote kwamba ckipo pamoja nao katika wakati huu mgumu unaowakabili na kwamba chama  kitashirikiana nao hadi ufumbuzi wa kudumu utakapopatikana.

Imeandikwa na Mwandishi wetu-Mbeya

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527