RAIS WA SIMBA SC, EVANS AVEVA NA MAKAMU WAKE GEOFREY NYANGE ‘KABURU’ WAPIGWA KALENDA NA KURUDI RUMANDE

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo July 31, 2017 imetoa siku saba kwa upande wa mashtaka ufanye jitihada za kukamilisha upelelezi wa kesi inayowakabili Rais wa Simba SC, Evans Aveva na Makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’.


Hatua hiyo imekuja baada ya Mwendesha Mashitaka wa TAKUKURU, Leonard Swai kudai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika.


Upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Mtakyamirwa Philemon ulidai mara ya nne sasa upande wa mashitaka unadai upelelezi haujakamilika na kudai wanatakiwa kuhakikisha wanakuwa makini na shauri hilo ili wakamilishe upelelezi kwani washitakiwa wako ndani kwa kosa lisilo na dhamana.


Hata hivyo, Swai alidai kuwa mashitaka ya kughushi wanahitaji upelelezi wa kina hivyo anaomba Mahakama kuwapa siku 14.


Hakimu Nongwa alisema Mahakama imezingatia hoja za pande zote mbili kwamba mashitaka ya kughushi yanachukua muda mrefu kukamilika na kusisitiza kuwa licha ya sheria kutaka kuahirishwa kwa kesi kusizidi siku 14 ombi la upande wa utetezi lina maana hivyo kutoa muda huo ili kama washitakiwa wana kosa watiwe hatiani.


Hakimu Nongwa aliahirisha kesi hiyo hadi August 7, 2017 kwa ajili ya kutajwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527